Mikopo kwa sekta binafsi imeendelea kuongezeka kwa kasi ya kuridhisha-Gavana Tutuba

NA GODFREY NNKO

MWENYEKITI wa Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) ambaye pia ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba amesema, mikopo kwa sekta binafsi imeendelea kuongezeka kwa kasi ya kuridhisha ikiwa ni takribani asilimia 17.1.
Ni kwa kipindi cha Julai hadi Septemba 2024, sawa na ukuaji uliofikiwa katika kipindi cha Aprili hadi Juni,2024.

Gavana Tutuba ameyasema hayo kupitia taarifa aliyoitoa leo Oktoba 3,2024 kwa umma wakati akielezea uamuzi wa Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) ya Bodi ya Wakurugenzi wa Benki Kuu ya Tanzania ambayo ilikutana Oktoba 2,2024.

Katika kikao hicho,MPC imeamua Riba ya Benki Kuu (CBR) kuendelea kuwa asilimia 6 kwa robo mwaka itakayoishia Disemba 2024.

"Aidha, ubora wa rasilimali za benki uliendelea kuongezeka ambapo uwiano wa mikopo chechefu ulipungua hadi asilimia 3.9 mwezi Agosti 2024, kutoka asilimia 5.1 katika mwezi kama huo mwaka 2023."

Pia,amesema mikopo kwa sekta binafsi inatarajiwa kuendelea kuongezeka, sambamba na kuimarika kwa uchumi wa dunia na wa hapa nchini.

Vilevile, amesema utekelezaji wa sera ya bajeti ulikuwa wa kuridhisha, ambapo mapato ya kodi yamevuka lengo, kufuatia kuimarika kwa usimamizi na kuongezeka ulipaji kodi kwa hiyari.

Amesema,Serikali imeendelea kupanga matumizi kulingana na mapato. "Deni la Taifa lilifikia dola za Marekani milioni 37,721.6, sawa na asilimia 46.9 ya Pato la Taifa (GDP), ambalo ni 3 chini ya kigezo cha mtangamano wa kiuchumi cha ukomo wa asilimia 60 kwa nchi za SADC."

Wakati huohuo,Gavana Tutuba ameeleza kuwa, uwiano wa deni kwa Pato la Taifa, kwa thamani halisi ya sasa (NPV) ulikuwa ni asilimia 36.4 mwaka 2023/24, chini ya kigezo cha mtangamano wa kiuchumi cha ukomo wa asilimia 50 kwa EAC.

Mbali na hayo amesema,sekta ya nje imeendelea kuimarika, sambamba na kupungua kwa athari za mitikisiko ya kiuchumi duniani.

"Nakisi ya urari wa malipo ya kawaida (current account deficit) inakadiriwa kupungua hadi kufikia asilimia 3.2 ya Pato la Taifa kwa mwaka ulioishia Septemba 2024 kutoka asilimia 4.4 ya Pato la Taifa katika kipindi kama hicho mwaka 2023.

"Mwenendo huu ulitokana na ongezeko la mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi, hususani utalii, dhahabu, tumbaku na korosho.

"Nakisi ya urari wa malipo ya kawaida inatarajiwa kuendelea kuimarika na hivyo kusaidia kupunguza mahitaji ya fedha za kigeni nchini."

Kwa upande wa Zanzibar,Gavana Tutuba amesema, urari wa malipo ya kawaida unakadiriwa kuwa ziada ya dola za Marekani milioni 507, ikilinganishwa na ziada ya dola za Marekani milioni 363.7 katika kipindi kama hicho mwaka 2023, kutokana na kuongezeka kwa utalii na kupungua kwa uagizaji wa bidhaa.

"Upatikanaji wa fedha za kigeni uliimarika katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2024, sambamba na msimu wa shughuli za utalii na mauzo ya mazao ya kilimo na biashara nje ya nchi.

"Kupanda kwa bei ya dhahabu katika soko la dunia pia kulichangia ongezeko la mapato ya fedha za kigeni nchini.

"Kutokana na mwenendo huu, kasi ya kuporomoka kwa thamani ya shilingi ilipungua hadi kufikia asilimia 10.1 kwa mwaka unaoishia Septemba 2024, kutoka asilimia 12.5 kwa mwaka ulioshia Juni 2024.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news