NA DIRAMAKINI
RAIS wa Simba Sports Club,Mohammed Dewji (MO) amesema, njia moja wapo ya kuifanya klabu hiyo kuwa na mafanikio makubwa ni pamoja na mashabiki wakiwemo wadau mbalimbali kudumisha umoja, ushirikiano na mshikamano.
Amesema,pia bila fitna na kuwa kitu kimoja bila kugawanyika kutaendelea kuijenga Simba inayoweza kushinda ubingwa wa Klabu Bingwa barani Afrika.
Dewji ambaye pia ni mwekezaji mkubwa katika klabu hiyo ameyasema hayo leo Oktoba 6,2024 jijini Dar es Salaam katika Mkutano wa Mwaka wa Simba Sports Club 2024.
“Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kutufikisha wote hapa na kwa niaba ya Wanasimba wote naomba kumpongeza Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu kwa uongozi wake bora na mchango wake mkubwa wa kuendeleza michezo nchini.
"Hii ni safari ya pamoja na kwa pamoja tutafanikisha maono makubwa, katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita Simba Sports Club imepata mabadiliko makubwa ambayo yanalenga kuimarisha klabu yetu.
“Huu ni wakati wa kuchukua hatua kwa nguvu zaidi, tukimaliza mchakato wa mabadiliko Simba itakuwa tayari kusimama imara na kujitegemea, kwa heshima kubwa naomba tuache fitna, tuache fitna tuwe kitu kimoja, tusigawanyike.
"Tukishirikiana tunaweza kujenga Simba inayoweza kushindana ubingwa wa Klabu Bingwa Afrika, malengo haya sio ndoto, bali ni lengo linaloweza kufikiwa, pamoja tunaijenga Simba ya kesho,”amesema Mohammed Dewji.