MPC yaridhia Riba ya Benki Kuu (CBR) kuendelea kuwa asilimia 6 kwa robo itakayoishia Disemba, 2024

NA GODFREY NNKO

MWENYEKITI wa Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) ambaye pia ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba amesema,Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) ya Bodi ya Wakurugenzi wa Benki Kuu ya Tanzania imeamua Riba ya Benki Kuu (CBR) kuendelea kuwa asilimia 6 kwa robo mwaka itakayoishia Disemba 2024.
Gavana Tutuba ameyasema hayo kupitia taarifa aliyoitoa leo Oktoba 3,2024 kwa umma ambapo amefafanua kuwa, uamuzi huo umefikiwa baada ya wajumbe wa kamati hiyo kukutana Oktoba 2,2024.

"Uamuzi huu ulitokana na matarajio ya mfumuko wa bei kuendelea kuwa chini ya lengo la nchi la asilimia 5."

Amesema kuwa, kamati pia inatarajia uchumi kuendelea kukua kwa kasi ya kuridhisha, sambamba na kuimarika kwa mazingira ya kiuchumi duniani na hapa nchini.

"Uchumi wa dunia unatarajiwa kuendelea kukua sambamba na kuimarika kwa mazingira ya upatikanaji fedha.

"Kutokana na hali hii, Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki ya Dunia wanakadiria uchumi wa dunia kukua kwa asilimia 3.2 na asilimia 2.6, mtawalia, mwaka 2024."

Mwenyekiti na Gavana Tutuba amebainisha kuwa,mwenendo huo unatarajiwa kuchagiza shughuli za uzalishaji hapa nchini.

Vile vile, amebainisha kuwa, mfumuko wa bei unatarajiwa kuendelea kupungua, ikiwa ni matokeo ya utekelezaji wa sera ya fedha inayolenga kupunguza ongezeko la ukwasi sambamba na kupungua kwa bei za bidhaa katika soko la dunia, hususan mafuta na mbolea.

"Kutokana na hali hii, benki kuu katika nchi nyingi zinatarajiwa kupunguza au kutokubadili riba zao za sera ya fedha. Vilevile, benki kuu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) zinatarajiwa kufuata mwenendo huu wa kisera."

Ameeleza kuwa,bei za bidhaa katika soko la dunia zimeendelea na zinatarajiwa kuendelea kuwa tulivu. Pia,katika robo ya mwaka inayoishia Disemba 2024, bei za mafuta ghafi zinatarajiwa kuwa kati ya dola za Marekani 72 hadi 82 kwa pipa, kutokana na ongezeko la uzalishaji.

"Hali hii inatarajiwa kupunguza ongezeko la mfumuko wa bei na mahitaji ya fedha za kigeni nchini kwa kuwa bidhaa za mafuta huchangia takriban asilimia 20 ya bidhaa zote zinazoagizwa kutoka nje ya nchi.

"Kamati pia ilitathmini utekelezaji wa sera ya fedha katika robo mwaka inayoishia Septemba 2024, pamoja na mwenendo na mwelekeo wa uchumi hapa nchini."

Gavana Tutuba amesema,kamati ilibaini kuwa utekelezaji wa sera ya fedha ulifanikiwa kuhakikisha mfumuko wa bei unabaki ndani ya lengo la asilimia 5.

"Katika robo ya kwanza ya mwaka 2024, uchumi ulikua kwa asilimia 5.6, huku shughuli za ujenzi, kilimo, fedha na bima, na usafirishaji zikichangia kwa kiwango kikubwa katika ukuaji huu.

"Kwa mujibu wa viashiria vya awali, uchumi unakadiriwa kukua kwa asilimia 5.8 na asilimia 5.6 katika robo ya pili na ya tatu ya mwaka 2024, mtawalia, na unatarajiwa kuendelea kukua katika viwango hivyo katika robo ya mwisho wa mwaka.

"Ukuaji huu utachangiwa na kuendelea kuimarika kwa mazingira ya kiuchumi hapa nchini na duniani. Kuendelea kuimarika kwa mazingira ya kiuchumi nchini kunatokana na maboresho katika biashara na uwekezaji, ikiwemo yanayoendelea kutekelezwa kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo."

Amefafanua kuwa,uzalishaji katika shughuli za kilimo unatarajiwa kuongezeka kwa kiwango kikubwa kutokana na matumizi ya pembejeo (mbolea na mbegu bora), viwatilifu na uwekezaji katika miradi ya umwagiliaji.

Vilevile, shughuli za ujenzi na usafirishaji zinatarajiwa kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi. Uchumi wa Zanzibar ulikua kwa asilimia 6.4 katika robo ya kwanza ya mwaka 2024, ukichochewa na shughuli za usafirishaji, fedha na bima, na ujenzi.

Pia, amebainisha kuwa,mfumuko wa bei uliendelea kuwa tulivu, ndani ya lengo la nchi na vigezo vya mtangamano wa kiuchumi katika jumuiya za kikanda.

"Mfumuko wa bei ulikuwa asilimia 3 na 3.1 mwezi Julai na Agosti 2024, mtawalia, na unatarajiwa kuwa asilimia 3.2 katika robo ya nne ya mwaka 2024."

Amesema, mfumuko wa bei unatarajiwa kuendelea kuwa tulivu, ukichangiwa na kupungua kwa bei za bidhaa katika soko la dunia, upatikanaji wa chakula cha kutosha na umeme wa uhakika, pamoja na utekelezaji wa sera madhubuti za fedha na kibajeti.

Kwa upande wa Zanzibar,Gavana mfumuko wa bei ulipungua hadi kufikia asilimia 5.1 kutokana na kushuka kwa bei bidhaa za chakula na zisizo za chakula.

"Hata hivyo, migogoro ya kisiasa Ulaya Mashariki na Mashariki ya Kati inaweza kusababisha kuvurugika kwa mnyororo wa ugavi na kupelekea kuongezeka kwa bei za bidhaa katika soko la dunia."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news