Mtaji wa NHC wafikia shilingi trilioni 5.16 hadi Juni,2024

NA GODFREY NNKO

MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Hamad Abdallah amesema kuwa, hadi kufikia Juni,2024 mtaji wa shirika hilo ulikuwa shilingi trilioni 5.16 ikilinganishwa na mwaka uliopita shilingi trilioni 5.04.Pia amesema, thamani na mali za shirika zinaendelea kukuwa mwaka hadi mwaka kutokana na usimamizi na maelekezo mazuri wanayopata kutoka serikalini na chama tawala.

Mkurugenzi Mkuu huyo ameyasema hayo leo Oktoba 13,2024 katika wasilisho lake kuhusu majukumu na mafanikio ya shirika hilo katika mkutano wa viongozi wa Jimbo la Ilala mkoani Dar es Salaam.
"Kwa mafanikio haya, maana yake chama kinachoisimamia Serikali kinafanya kazi yake. Na ndani ya shirika la nyumba tunafanya vizuri."

Amesema, jitihada za shirika katika kuwekeza na kutekeleza miradi mbalimbali imekuwa ikiwezesha Serikali kupata kodi na gawio kubwa.

"Katika kipindi cha miaka mitano (2018/19-2022/2023) Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) liliweza kulipa kodi mbalimbali na gawio Serikalini zinazofikia shilingi bilioni 134.55."
Katika hatua nyingine amesema kuwa, ndani ya miaka mitano kuanzia 2018/19-2023/24 mapato ya shirika yamekuwa kutoka shilingi bilioni 125 kwa mwaka hadi shilingi bilioni 184 kwa mwaka sawa na ongezeko la asilimia 47 kwa mwaka.

"Mapato ya mwaka 2023/24 ambayo yanaendelea kukaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali yamefikia shilingi bilioni 184."

Aidha, amewaeleza viongozi hao kuwa, majukumu ya shirika hilo yanatekelezwa kwa kuzingatia Mpango Mkakati wa Miaka 10 wa NHC ambao ulianza 2015/16 -2024/2025.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mkuu huyo amesema kuwa, Ilala ni miongoni mwa maeneo nchini ambapo shirika hilo linatekeleza miradi mingi ya kihistoria kupitia Sera ya Ubia na tayari matokeo yameanza kuonekana.

"Ilala inakwenda kuwa kama Dubai. Tunajenga miradi ambayo inazingatia kasi na viwango vya Kimataifa. Tukijipa miaka 10 ijayo Ilala itakuwa imejipa historia ya kutoonekana majengo mabovu."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news