WASHINGTON D.C-Benki ya Dunia imemchagua Mtanzania, Dkt. Zarau Wendeline Kibwe, kuwa Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Benki hiyo atakayesimamia Kanda Namba Moja ya Afrika inayojumuisha nchi 22 ikiwemo Tanzania, nafasi ambayo Tanzania imewahi kuihudumu miaka 54 iliyopita.


Akizungumza jijini Washington D.C, baada ya kutangazwa kuchukua nafasi hiyo, Dkt. Zarau Wendeline Kibwe amesema kuwa ataitumia nafasi hiyo kusimamia uendeshaji wa Benki na Taasisi zake Pamoja na kutetea Maslahi ya nchi katika Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Dunia pamoja na maslahi ya Kanda ya Afrika anayoisimamia ili kukuza maendeleo na uchumi wa nchi hizo.
Akizungumza kwa niaba ya Serikali katika Mkutano huo uliomtangaza Dk. Kibwe kuchukua nafasi hiyo, Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, anayeongoza Ujumbe wa Tanzania katika Mikutano hiyo ya Mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa – IMF na Benki ya Dunia, amesema kuwa hayo ni matokeo ya juhudi za Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anavyoifungua nchi na kukuza Diplomasia ya Kimataifa.
Dkt. Nchemba amempongeza Dkt. Kibwe kwa kupata nafasi hiyo na kwamba kutokana na umahili wake katika masuala ya uchumi na fedha, pamoja na uzoefu wake wa muda mrefu katika Ofisi hiyo, anaamini kuwa maslahi ya nchi yataendelea kulindwa ipasavyo kwa manufaa ya watanzania.
Dkt. Zarau Wendeline Kibwe ni mchumi wa kitanzania ambaye hivi karibuni amechaguliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia kwa Kanda Namba Moja ya Afrika inayojumuisha nchi za Botswana, Burundi, Eritrea, Eswatini, Ethiopia, Gambia, Kenya, Lesotho, Liberia, Malawi, Msumbiji, Namibia, Rwanda, Shelisheli, Sierra Leone, Somalia, Sudan Kusini, Sudan, Tanzania, Uganda, Zambia, na Zimbabwe.


Alipata Shahada yake ya Kwanza ya Sayansi katika Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe kilichopo Morogoro, Tanzania.
Tags
Benki ya Dunia Tanzania
Dr Mwigulu Lameck Nchemba
Dr Zarau Wendeline Kibwe
Habari
Kimataifa
World Bank