ZANZIBAR-Naibu Waziri wa Maendeleo wa Jamii Jinsia Wazee na Watoto Zanzibar,Mheshimiwa Anna Athanas Paul amesema iwapo mtoto wa kike atasoma kwa bidii ataweza kuviepuka viashiria vya unyanyasaji ambavyo ndio vikwazo vikubwa vinavyowafanya kutokufikia malengo yao.
Mhe. Anna ameeleza hayo katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike huko katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) Kampasi ya Maruhubi, Unguja.
Amesema, watoto wa kike wakisoma kwa bidii itasaidia kutimiza malengo yao ya baadae, hali ambayo itasaidia kujiepisha na vitendo viovu ikiwemo unyanyasaji wa kijinsia.
“Iwapo mtoto wa kike atasoma kwa bidii ataweza kuviepuka viashiria vya unyanyasaji ambavyo ndio vikwazo vikubwa vinavyowafanya kutokufikia malengo yao,” amesema Waziri huyo.
Naibu Waziri huyo amefahamisha kuwa,kwa mujibu takwimu kutoka Afisi ya Mtakwimu Mkuu mwaka 2023 matukio 1954 ya ukatili na udhalilishaji yaliripotiwa kati ya matukio hayo wasichana walikuwa 1,263 sawa na aslimia 77.1 hiyo inaonesha bado watoto wa kike wanahitaji elimu kwa nguvu zote.
Kwa upande wa watoto walioshiriki katika maadhimisho hayo akizungumza Fatma Salum (16) kutoka Skuli ya Msingi ya Tumekuja amesema ni vyema wazazi na walezi wakatenga muda maalum wa kuzungumza na watoto ili kuyajua mambo yanayowakwaza katika mazingira yanayowazunguka.
Naye Mtaalam wa elimu kutoka Shirika la Kusaidia Watoto Duniani Kanda ya Tanzania, Bw.Henry Tindwa amesema,Save the Children itaendelea kusaidia watoto kujielewa ili kupunguza wimbi la udhalilishaji na watoto kujielewa.
Siku ya mtoto wa kike huadhimishwa kila mwaka ifikapo Oktoba 11 na kauli mbiu ya mwaka huu ni "Muezeshe mtoto wa kike,apaze sauti yake".