GEITA-Shirika la Taifa la Nyumba (NHC) ni miongoni mwa taasisi,mashirika ya umma na wadau wengine zaidi 600 wanaoshiriki katika Maonesho ya Saba ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika viwanja vya Bombambili mkoani Geita.
Maonesho hayo yenye kauli mbiu ya "Matumizi ya Teknolojia Sahihi ya Nishati Safi katika Sekta ya Madini kwa Maendeleo Endelevu” yalianza Oktoba Oktoba 3,2024 huku yakitarajiwa kufikia tamati Oktoba 13,2024.
NHC kupitia maonesho hayo wamekuja kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma wanazotoa ikiwemo kuuza bidhaa zao.
Afisa Mauzo na Masoko wa NHC, Ahmad Mwangu amesema,miongoni mwa huduma ambazo shirika huwa linatoa ni kupangisha nyumba,kuuza nyumba za kipato cha chini ambazo ni rahisi na zenye ubora wa hali ya juu, ambazo zipo mikoa yote ya Tanzania.
Nyumba hizo zinajumuisha za Iyumbu Satellite Center jijini Dodoma, kipato cha kati ni pamoja na Samia Housing Scheme eneo la Kawe Tanganyika Packers jijini Dar es Salaam.
Zingine ni Medeli Phase III jijini Dodoma na kipato cha juu ni Kawe Seven Eleven (7/11) na Morocco Square jijini Dar.
Pia,NHC wana viwanja wanauza eneo la Burka Mateves jijini Arusha,Commercial Complex (majengo ya kibiashara) Zongomela Kahama mkoani Shinyanga, Mtanda-Lindi, Masasi-Mtwara, Mutukula-Kagera hizi ni baadhi ila yapo majengo mengi.