NHIF yajipanga kuwafikia wananchi wote

DODOMA-Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umejiwekea mikakati thabiti kuhakikisha unafikisha elimu na umuhimu wa kujiunga na bima ya afya kwa wananchi wote nchini.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,Mhe. Dotto Biteko akiambatana na Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama wakipata maelezo ya huduma za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kutoka kwa Kaimu Meneja wa Kitengo cha Uhusiano wa NHIF, Bi. Grace Kisinga, hususani maandalizi ya utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote alipotembelea banda la NHIF, kwenye Mkutano Mkuu wa Wataalam wa Maabara unaoendelea katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete uliopo Dodoma.

Kaimu Meneja wa Kitengo cha Uhusiano wa NHIF, Bi. Grace Kisinga ameyasema hayo leo Oktoba 2,2024 alipokua akitoa maelezo kwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,Mhe.Dotto Biteko alipotembelea banda la NHIF.

Ni katika kongamano la wataalamu wa maabara linalofanyika katika Ukumbi Mikutano wa Jakaya Kikwete (JKCC) Dodoma.

Mbali na hilo ameeleza kuwa, mfuko umejiandaa katika kutoa elimu kwa wananchi ili kuhakikisha kwamba dhana ya bima ya afya kwa wote inaeleweka kwa wananchi na kuweza kujiunga na kutimiza azma ya Serikali ya bima ya afya kwa kila mtu.

Pamoja na hayo NHIF imejipanga kuwafikia wananchi hususani waliopo ngazi za chini na kuhakikisha kuwa inajenga uelewa kwa wananchi kwa kutumia ofisi zilizopo katika mikoa yote na kuwafikia wananchi hasa waliopo katika maeneo ya pembezoni.

Aidha, mfuko umeandaa mpango wa elimu wa kuwezesha kupeleka elimu hiyo kwa urahisi, lakini pia kutumia fursa za kukutana na wananchi katika maonesho na kufanya kampeni ya kata kwa kata.

Lengo ni kuhakikisha kila mtanzania anapata elimu ya dhana ya bima ya afya katika maeneo yao.

“Tutatumia njia mbalimbali kutoa elimu ikiwa ni pamoja na mikutano na maonesho mbalimbali ikiwa ni pamoja na wiki ya uwekezaji katika sekta ya madini Geita itakayofanyika Geita na sherehe za kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mkoani Mwanza."

Hata hivyo, mfuko umejipanga kuhakikisha uimara wa bima ya afya na kuhakikisha kuwa wananchi wanaelewa na kujiunga kabla ya kuugua ili pindi anapopata changamoto awe na uhakika wa matibabu kwa sababu ugonjwa unakuja bila taarifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news