RUVUMA-Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) imekabidhi mtambo wa umwagiliaji wenye thamani ya shilingi 4,236,000 kwa bwana Jacob Davis na wenzake wawili wanaojishughulisha na kilimo cha umwagiliaji ambapo kwa sasa wamejikita kuzalisha vitunguu katika Kijiji cha Nakahengwa katika Halmashauri ya Songea Vijijini mkoani Ruvuma.
Akikabidhi vifaa hivyo kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe, Mkuu wa Wilaya ya Songea, Mhe. Kapenjama Ndile amesema, Waziri wa Kilimo aliahidi kuwasaidia vijana hao mnamo Septemba 17, 2024 alipotembelea shamba lao akiwa ameongozana na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji,Bw. Raymond Mndolwa pamoja viongozi wengine.
Waziri Bashe alivutiwa na kilimo hicho ambapo vijana hao walieleza changamoto zinazowakabili katika kilimo hicho ikiwa ni pamoja na kukosa miundombinu ya uhakika ya umwagiliaji hali inaypelekea kushindwa kutanua wigo wa kulima mashamba makubwa kutokana na hali duni ya kiuchumi.
Awali wakulima hao vijana walikuwa wakilazimika kutumia jenereta bovu kuvuta maji ya kumwagilia shamba hilo.inaelezwa kuwa jenereta hilo wakati mwingine lilikuwa na changamoto ya kushindwa kuwaka na kupelekea vitunguu kushindwa kustawi.kutokana na ukosefu wa maji.
Baada ya Waziri Bashe alipita katika kijiji hicho na kujionea shamba hilo na alimwagiza Mkurugenzi Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Bw. Raymond Mndolwa kuwanunulia vijana hao mtambo ambao umekamilika kila kitu na leo ahadi hiyo imetimia kwa vijana kupatiwa mtambo wenye thamani ya zaidi ya million 4.24 tayari kwa matumizi ya kuendeleza kilimo cha umwagiliaji.
Hata hivyo, akisoma taarifa fupi ya kukabidhi vifaa hvyo, Mhandisi Umwagiliaji mkoa wa Ruvuma,Mhandisi Lucy Chaula amesema mtambo huo umejumuisha Engine diesel 24 HP- pc 1, Water pump -pc 1, Delivery pipe 300m, Sunction pipe, pamoja, Sprinkler -pc 1, Cremps pamoja na Reli za engine- pc1.
Kwa sasa vijana hao wanalima ekari 3 za vitunguu na soko lao kubwa ni mji wa Songea na Mbinga.ambapo mji wa Songea pekee unahitaji tani 50 za mbogamboga kwa siku lakini baada ya kupata mtambo huo wameahidi kutanua zaidi shamba lao lengo ikiwa ni kuvuna zaidi ili waweze kulisha nchi nzima.