Nitaendelea kufanya mageuzi makubwa katika sekta mbalimbali nchini-Rais Dkt.Mwinyi

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameahidi kufanya mageuzi makubwa ya kuboresha mandhari ya Zanzibar kwa kujenga barabara za juu kutoka Uzi na Ng’ambwa Kaskazini Unguja hadi Charawe – Chwaka, Mkoa wa Kusini Unguja ili kurahisisha usafiri na usafirishaji kwa mikoa hiyo.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo Oktoba 26,2024 alipofungua soko jipya la ghorofa mbili Mwanakwerekwe, Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi, ikiwa ni mwendelezo wa mafanikio ya miaka minne ya uongozi wa awamu ya nane ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar anayoiongoza.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ameahidi kurahisisha huduma za usafiri wa umma kwa kuziagiza mamlaka zinazohusika kujenga vituo vikubwa vya mabasi vitakavyoruhusu mwingiliano wa moja kwa moja baina ya masoko ya Kwerekwe, Jumbi, na Chuini, ili kutoa fursa kwa wananchi na wafanyabiashara kunufaika na masoko hayo.

Halikadhalika, Rais Dkt.Mwinyi amewaahidi Wazanzibari kuibadili Zanzibar kuwa kituo bora cha biashara cha kimataifa kwa kutoa fursa za mwingiliano wa wafanyabiashara kutoka mataifa mbalimbali kuja nchini, kuuza na kununua bidhaa.

Katika hatua nyingine, Rai Dkt. Mwinyi amezitaka mamlaka zinazohusika na Soko la Mwanakwerekwe kutowatoza ushuru mkubwa wafanyabiashara wa eneo hilo, akibainisha kuwa fedha zilizotumika kujenga soko hilo hazikutokana na mkopo bali ni kodi za wananchi wenyewe, hivyo Serikali haitegemei chochote kutoka kwa wananchi na wafanyabiashara wa soko hilo isipokuwa kusaidia kuliendesha na kulitunza soko.
Vilevile, Rais Dkt. Mwinyi aliwaahidi wafanyabiashara wadogo na wajasiriamali sokoni hapo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwaongezea mitaji ya biashara zao endapo watajiunga kwa makundi ili kupata mikopo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news