NA GODFREY NNKO
MFUKO wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeendelea kurekodi mafanikio makubwa katika uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Hayo yamesemwa leo Oktoba 13,2024 na Robert Kadege ambaye ni Meneja wa Huduma kwa Wateja wa NSSF katika mkutano wa viongozi wa Jimbo la Ilala mkoani Dar es Salaam.
Ni wakati akiwasilisha wasilisho la umuhimu wa hifadhi ya jamii na kikokotoo cha pensheni katika mkutano huo.
Amesema,kuanzia Machi 2021 hadi Juni 2024 mfuko huo umesajili jumla ya wanachama 694,503.
"Aidha,mwezi Machi mfuko ulikuwa na thamani ya shilingi trilioni 4.8 na ilipofika Juni,2024 thamani ya mfuko ilifikia shilingi trilioni 8.6."Pia, amesema kuwa uhimilivu wa mfuko huo ni asilimia 90 na kiwango cha chini cha uhifadhi kwa mujibu wa viwango vya Kimataifa ni asilimia 40.
Hata hivyo, ameendelea kuwahimiza waajiri kuwasilisha kwa wakati michango ya wanachama ili kila mwanachama aweze kupata stahiki zake pale zitakapohitajika.