PWANI-Kampuni ya ukopeshaji mikopo ya OYA MICROCREDIT imesema imehuzunishwa na taarifa mbalimbali zinazohusu tukio la kusikitisha lililosababisha kifo cha mfanyabiashara na mkazi wa Mbagala Mlandizi, Kibaha mkoani Pwani, Juma Mfaume (40) wakati wafanyakazi wake walipokwenda kudai mkopo nyumbani kwake.
Kampuni hiyo imetoa kwa familia ya Mfaume na kwa jamii nzima katika hiki kipindi kigumu na kwamba inapenda kuweka wazi kwa Watanzania na jamii kwa ujumla kuwa, haijawahi kuidhinisha wala kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wake kutumia aina yoyote ya nguvu katika urejeshaji wa madeni.
“Taratibu zetu ni za kisheria na zinazingatia maadili na tukio hili halioneshi maadili au taratibu zetu za kawaida za uendeshaji, OYA inashirikiana kikamilifu na Mamlaka katika uchunguzi wao na tutaendelea kuheshimu sheria na kudumisha uwazi katika mchakato huu mzima.
"Taratibu zetu za urejeshaji wa madeni zinalenga kuwa za heshima na kufuata sheria na tunachukua hatua za haraka kupitia upya na kuimarisha michakato yetu ya ndani ili kuhakikisha kuwa tukio kama hili halitokei tena.
“Tunaendelea kujitolea kwa dhamira yetu ya kusaidia na kuwawezesha Watu wenye kipato cha chini, na tutaendelea kufanya kazi ili kudumisha imani ya Wateja wetu na jamii tunazozihudumia."