ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali itaendelea kuimarisha uhuru wa kuabudu na kuziagiza taasisi za kidini kuendelea kuiombea nchi amani na umoja.
Rais Dkt.Mwinyi amesema kuwa,taasisi za kidini zina wajibu mkubwa wa kushirikiana na Serikali na kuunga mkono juhudi za kuleta Amani,Umoja na Mshikamano wa Watanzania.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Oktoba 27, 2024 alipozungumza katika Maombi maalum ya kumpongeza Mhashamu Askofu Augustine Ndeliakyama Mweleli Shao, C.S.Sp kwa utume wake katika Kanisa Katoliki Jimbo la Zanzibar na maombi kwa Taifa iliyofanyika Viwanja vya Mao Tse Tung Mkoa wa Mjini Magharibi.
Rais Dkt.Mwinyi amesisitiza kuwa,Serikali inathamini mchango mkubwa unaotolewa na Kanisa Katoliki Jimbo la Zanzibar,kwani umekuwa msaada muhimu wa kuimarisha ustawi wa jamii katika nyanja mbalimbali.
Akizungumzia ukarabati wa Kanisa la Minara miwili unaotarajiwa kutekelezwa na Kanisa hilo kuwa ni kuunga mkono juhudi za Serikali na Shirika la Elimu Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa(UNESCO) la kuimarisha Mji Mkongwe wa Zanzibar ambao ni Urithi wa Dunia.
Halikadhalika Rais Dkt.Mwinyi amechangia shillingi Milioni 100 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amechangia shilingi Milioni 50 kwa ajili ya ukarabati wa Kanisa la Mtakatifu Joseph liliopo Shangani Wilaya ya Mjini.