DOHA-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi leo katika siku ya kwanza ya ziara yake nchini Qatar amekutana na Waziri wa nchi wa Qatar anayeshughulikia masuala ya Nishati, Mheshimiwa Saad bin Sherida Al- Kaabi.
Mazungumzo yao yametoa nuru kwa Qatar kuiuzia Tanzania mbolea aina ya Urea kwa gharama nafuu.
Mazungumzo hayo alihudhuriwa pia na Balozi wa Tanzania nchini Qatar, Mheshimiwa Habib Awesi Mohammed pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mbolea ( TFC ),Samwel Ahadi Mshote.
Kesho akimaliza ziara yake nchini Qatar, Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi anatarajiwa kushiriki mkutano mkubwa wa Kimataifa wa kutimiza miaka 30 ya Familia Duniani utakaofanyika jijini Doha.
Halikadhalika Mkutano huo unafuatia Azimio la mwaka 1994 la Umoja wa Mataifa la Mwaka wa Kimataifa wa Familia ( IYF ) lililopitishwa rasmi na Baraza la Umoja wa Mataifa likizingatia thamani na umuhimu uliopo wa kuzilinda na kuzisaidia familia kupitia sheria za Kimataifa.
Vilevile maazimio ya mwaka wa Kimataifa wa Familia hufanyika kila baada ya miaka kumi.