Rais Dkt.Mwinyi azindua tawi la PBZ Mwanza, asema itaendelea kuchochea fursa za uchumi kwa wananchi

MWANZA-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameeleza kuwa hatua ya Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) kufungua matawi inaongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi wa kada mbalimbali, na amewahimiza wananchi wa Mwanza kuitumia PBZ kupanua wigo wa biashara zao kupitia mikopo inayotolewa na benki hiyo.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 13 Oktoba 2024 alipozindua tawi la Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ), lililopo Wilaya ya Nyamagana, Mwanza.

Rais Dkt. Mwinyi ameongeza kuwa PBZ ni taasisi ya kifedha inayomilikiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, na ni benki inayovutia wananchi wengi kutokana na huduma zake pamoja na unafuu wa mikopo.

Amefahamisha kuwa kuendelea kufanya vizuri kwa benki hiyo kunatokana na mtaji wake unaofikia trilioni 2.3, huku ikiwa benki inayofanya biashara ya zaidi ya shilingi trilioni 1, na kuwa miongoni mwa benki saba bora nchini.
Rais Dk. Mwinyi amesema kuwepo kwa Benki ya PBZ Tanzania Bara ni daraja muhimu la kuunganisha Muungano kwa vitendo.

Vilevile amesema hatua hiyo inaonesha jinsi Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inavyotoa ushirikiano katika masuala ya kifedha kwa Zanzibar.

Halikadhalika amewahakikishia wananchi kuwa PBZ ni benki inayoaminika kutokana na uadilifu wa watendaji wake na usimamizi bora wa masuala ya kifedha.

Ameelezea udhamini wa PBZ wa Ligi Kuu ya Zanzibar na michezo mingine, pamoja na misaada katika sekta za elimu, afya, na michezo ni ishara ya jinsi benki hiyo ilivyojipanga kuisaidia jamii, na ameihimiza kuendelea na misaada hiyo.
Rais Dk. Mwinyi amewahimiza wananchi wa Mwanza kuitumia PBZ kwa kufungua akaunti na kuchangamkia fursa za mikopo ili kuinuka kiuchumi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news