Rais Dkt.Mwinyi azungumza na mabalozi mbalimbali Afrika, asisitiza fursa za kiuchumi na kuitangaza Zanzibar

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi amewasisitiza Mabalozi wa Nchi za Afrika wanaoziwakilisha nchi zao nchini Tanzania kuimarisha ushirikiano na fursa za kiuchumi pamoja na kuutangaza utalii wa Zanzibar kimataifa.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Oktoba 21, 2024 alipozungumza na mabalozi hao waliotembelea Ikulu baada ya kumaliza ziara yao ya siku tatu ya kuitembelea Zanzibar, kuangalia fursa za uwekezaji na maeneo ya ushirikiano ambayo nchi hizo za Afrika zinaweza kufanya kazi na Zanzibar.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amesema wakati umefika kwa nchi za Afrika kuungana na kutumia rasilimali tulizonazo kuinua uchumi wetu na kubadilishana uzoefu ili kufikia maendeleo.

Halikadhalika, Rais Dkt. Mwinyi amewataka mabalozi hao kuangalia fursa za ushirikiano na uwekezaji, hususan katika sekta za utalii, usafiri wa baharini na usafirishaji, uvuvi na ufugaji wa vifaranga vya samaki, mafuta na gesi, na kilimo cha viungo ambacho Zanzibar ina utajiri mkubwa.
Akizungumzia sekta ya usafiri wa baharini na usafirishaji, amewataka mabalozi hao kuangalia fursa zilizopo kwenye sekta hiyo kwa kuziunganisha nchi za Afrika zilizo katika ukanda wa Bahari ya Hindi, kwani kwa pamoja nchi hizo zina uwezo wa kufanya biashara kubwa iwapo sekta hiyo itaimarishwa.
Akizungumzia suala la mafuta na gesi, Rais Dk. Mwinyi amewaeleza mabalozi hao kwamba Zanzibar imebaini kuwa na kiwango kikubwa cha gesi, na tayari imeanza mchakato wa kugawa vitalu kwa ajili ya kuvuna rasilimali hiyo.

Mabalozi hao wanatoka Burundi, Comoro, Kenya, Malawi, Misri, Morocco, Sudan, Rwanda, Uganda, na Zambia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news