Rais Dkt.Mwinyi mgeni rasmi maadhimisho Siku ya Wazee Duniani

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mheshimiwa Dkt.Hussein Mwinyi anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya wazee duniani yanayotarajiwa kufanyika Oktoba 7,2024 katika Uwanja wa Tibirinzi Pemba Mkoa wa Kusini.
Akitoa taarifa kuhusiana na siku hiyo Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,Mhe. Riziki Pembe Juma amesema, maadhimisho hayo huadhimishwa kila ifikapo Oktoba Mosi, lakini kwa mwaka huu itafanyika Oktoba 7 kutokana na sababu zisizoweza kuepukika.

Amesema, siku hiyo imeanza kuadhimishwa mwaka 1991 baada ya Baraza kuu la Umoja wa Mataifa kupitisha azimio nambari 45 ambalo lilitenga siku maalum ya kutambua na kutathmini michango na jitihada mbalimbali za wazee nchini.

Aidha,amefahamisha kuwa siku hiyo pia hutambua changamoto zinazowakabili katika maeneo ya wazee na kutoa fursa ya kutoa mawazo katika kutafakari namna ya kukabiliana na changamoto hizo ili kuhakikisha ustawi wa wazee unaimarika.

Aidha,Waziri Pembe amesema, kwa kutambua umuhimu wa wazee Serikali ya Awamu ya nane chini ya uongozi wake Dkt.Hussein Ali Mwinyi imeamua kuweka wizara hiyo ili kila mmoja katika jamii kupata haki na kutimiza wajibu wao ikiwemo wazee.

Ameongeza kuwa,katika kuadhimisha siku hiyo Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia na Watoto imeandaa usafiri wa kuwachukua na kuwarejesha katika wilaya zote Pemba ambapo kwa upande wa Unguja kutakuwa na wawakili watakaokwenda Pemba kuwawakilisha wazee walioko Unguja.

Hata hivyo, amefahamisha kuwa Serikali inaendeleza jitihada za kuwahudumia na kuwatunza wazee wasio na ndugu wala jamaa katika makao maalumu ya wazee yaliyopo Sebleni na Welezo kwa Unguja na Limbani kwa upande wa Pemba.

Katika maadhimisho hayo kaulimbiu ya mwaka huu ni Kuzeeka kwa Heshima Umuhimu wa Kuimarika Matunzo na Mifumo ya Usaidizi wa Wazee duniani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news