ARUSHA-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amerejesha eneo la Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Arusha, ambalo lilichukuliwa na Halmashauri ya Jiji la Arusha na kuagiza fedha Shilingi milioni 500 zilizokuwa zimetolewa na kanisa kwa ajili ya kununua tena eneo hilo na warejeshewe.
Agizo hilo lilitolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan baada ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha,Paul Makonda, kuwasilisha maombi hayo ya kanisa wakati wa kuhitimisha ziara yake mkoani humo.
Mhe. Mchengerwa amesema Rais ameelekeza Uongozi wa Mkoa wa Arusha na Halmashauri ya Jiji la arusha, kurejesha eneo hilo kwa kanisa mara moja pamoja na fedha hizo walizokuwa wametoa kwa ajili ya kununua eneo lao wenyewe.
“Nimekusikia Mkuu wa mkoa umezungumza kwa hisia sana,umeeleza kwa masikitiko namna ambavyo eneo la kanisa katoliki walilolimiliki muda mrefu,likanyang’anywa sijui kwa utaratibu upi.
“Na baadaye wakatakiwa kulilipia na fedha za michango zimetolewa Shilingi milioni 500 ili kufidia eneo hilo na bahati nzuri eneo hili nimekuwa nikilifuatlia kwa karibu,na jana nilizungumza na Rais na kumueleza changamoto hii,akanipa haya maelekezo.
“Rais amenielekeza eneo hilo lirejeshwe kwa kanisa mara moja na shilingi milioni 500 ambayo mliichukua kwa kanisa zirejeshwe mara moja na hili niwaelekeze mkoa kulisimamia kuhakikisha fedha hizi zinarudi kwa kanisa kama ambavyo namna mlizuchukua kutoka kanisani,”alisisitiza.
Awali akiwasilisha ombi hilo la Kanisa, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Makonda alisema alikuta mgogoro huo na kuwa baada ya kukaa ndani walikuta mambo waliyodhani ndiyo kumbe siyo.
“Fikiria licha ya eneo hilo kumilikiwa na kanisa awali ila nilikaa na Askofu akaniambia wameambiwa walipie na kupewa deadline na vitisho wakaamua kulipia kwa kutumia michango ya ujenzi na fedha ikakusanywa jimbo zima.
“Nilijisikia vibaya sana, nakuomba Waziri ile ni sadaka tusile sadaka warudishiwe fedha na eneo lao."