KAZAN-Rais wa China Xi Jinping amefanya mazungumzo ya faragha na mwenyeji wake Rais wa Urusi, Vladimir Putin huku wakiangazia zaidi kuhusu mzozo wa Ukraine na mahusiano kati ya nchi wanachama wa Kundi la Mataifa yanayoinukia Kiuchumi Duniani (BRICS) na nchi za Magharibi.
BRICS ambayo inaundwa na nchini wanachama ikiwemo Brazil, Urusi, India, China, Afrika Kusini, Iran, Misri, Ethiopia na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), uliasisiwa June 16,2009 na mataifa ya Urusi,China, India na Brazil.
Rais Xi amemwambia Putin kuwa, ulimwengu uko katika hali ya sintofahamu, lakini urafiki wao wa kimkakati utadumu hadi kwa vizazi vijavyo.
Msemaji wa Ikulu ya Kremlin Dmitri Peskov amesema, kwa kuwa mataifa ya Magharibi yanashambulia maslahi ya Urusi na China,hivyo ni wazi kwamba viongozi hao wawili walikuwa na mengi ya kuzungumza na kusisitiza kuwa Moscow na Beijing zina mtazamo sawa linapokuja suala la siasa za kimataifa.
Mkutano wa 16 wa kilele wa jumuiya ya BRICS ulioanza Jumanne mjini Kazan nchini Urusi unatarajiwa kupitisha maazimio muhimu kuhusu ushirikiano wa kifedha utakaokwepa mfumo wa SWIFT unaotawaliwa na Marekani.