MOROGORO-Imeelezwa kuwa, Majiko Banifu yanayotolewa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika Maonesho ya Samia KILIMO Biashara Expo 2024 yanapatikana kwa gharama nafuu, yanatunza mazingira, yanadumu na rafiki kwa afya ya watumiaji.

Hayo yamebainishwa leo Oktoba 6, 2024 na Mkuu wa wilaya ya Gairo, Mhe Jabir Makame wakati akizungumza na wananchi alipotembelea banda la REA yanapofanyika maonesho hayo kwa msimu wa tatu mwaka huu kijiji cha Leshata wilaya ya Gairo mkoani Morogoro.
Mhe. Makame ameeleza kuwa, majiko banifu ni rafiki na salama kwa afya ya watumiaji nchini na kuwasisitiza wananchi wake wayatumie kwa kuwa yanauzwa na kupatikana kwa bei rafiki.

Amesema,Gairo inatekeleza kampeni ya URITHI WA KIJANI yenye lengo la kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi ambayo yana athari katika Sekta ya Kilimo na Mifugo.

Naye, Mhandisi wa REA, Deusdedith Malulu ameongeza kuwa, majiko hayo yanatunza mazingira kwa kutumia kiasi kidogo cha mkaa na ufanisi wake ni mkubwa.
"Majiko haya hayaruhusu hewa ya mkaa ambayo ni hatari kwa watumiaji kutoka nje kwa aina ya muundo wake na hivyo kuwa rafiki kwa mazingira,"amesema Mhandisi Maluku.