GABORONE-Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (𝗦𝗔𝗗𝗖) inaendesha mafunzo kwa Ujumbe wa Uangalizi wa Uchaguzi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC Electoral Observation Mission - SEOM) katika uchaguzi Mkuu wa Botswana unaotarajiwa kufanyika tarehe 30 Oktoba, 2024.
Mafunzo hayo maalum kwa Ujumbe wa SEOM yanafanyika jijini Gaborone, Botswana kuanzia tarehe 17 hadi 20 Oktoba 2024 ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya uangalizi wa Uchaguzi Mkuu katika Jamhuri ya Botswana.
Tanzania ambaye ni Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC inaongoza ujumbe wa waangalizi hao ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tazania na Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amemteua Waziri Mkuu Mstaafu wa Tanzania Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda kuongoza Misheni hiyo ya uangalizi katika Uchaguzi Mkuu wa Jamhuri ya Botswana.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo yaliyofanyika tarehe 17 Oktoba, 2024 kwa niaba ya Ofisi ya Mratibu wa Masuala ya SADC Tanzania Bi. Lilian Mukasa amezishukuru Nchi Wanachama kwa kutuma wajumbe wao kwa ajili ya kuunda timu ya uangalizi ya SADC na kubainisha kuwa mafunzo hayo yataendeshwa na wakufunzi kutoka Sekretarieti ya SADC na Taasisi ya Uchaguzi kwa Demokrasia Endelevu Afrika (EISA).
Ameeleza kuwa mafunzo hayo yatajikita katika masuala ya mbalimbali ya kisera na kisheria ya Botswana, kikanda na kimataifa yanayotumika katika kusimamia uchaguzi ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha demokrasia na utawala bora katika kanda.
Amesema mafunzo hayo yatawapatia waangalizi maarifa na kuwawezesha kufahamu viwango na kanuni za uchaguzi wa kidemokrasia; Kanuni na Miongozo ya SADC inayoongoza Uchaguzi wa Kidemokrasia iliyorekebishwa; uangalizi wa uchaguzi katika hali za dharura za afya ya umma (mfano janga la COVID-19); kukuza uelewa kuhusu mzunguko wa uchaguzi; tathmini ya hatua za mzunguko wa uchaguzi; mifumo ya uchaguzi katika kanda ya SADC; ujuzi wa ukusanyaji taarifa; na matumizi ya kompyuta kibao, pamoja na ukusanyaji na utumaji wa taarifa (data).
Katika Uchaguzi mkuu huo wananchi wa Botswana watawachagua Wabunge wa Bunge la 13 la nchi hiyo na wajumbe wa Mabaraza ya Mitaa ambapo viti 61 vya Bunge la Taifa na viti 609 vya mabaraza ya mitaa vitashindaniwa. SEOM inatarajiwa kupeleka waangalizi wa uchaguzi katika wilaya, miji na majiji yote nchini Botswana.