MANYARA-Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu imesema itaendelea kuimarisha masuala ya menejimenti ya maafa kwa lengo la kuimarisha ustahimilivu dhidi ya maafa nchini.Kauli hiyo imetolewa Oktoba 7, 2024 wilayani Hanang’ mkoani Manyara na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi wakati akifungua Kikao Kazi cha Kukabidhi Nyaraka za Usimamizi wa Maafa za Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’ pamoja na kupokea Taarifa ya Tathmini ya Jiolojia, Haidrolojia na Mazingira.Dkt. Yonazi amesema miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuwekwa kwa mfumo wa kisera, kisheria na kitaasisi wa utaratibu wa masuala ya maafa kwa kutunga Sera ya Taifa ya Menejimenti ya Maafa ya mwaka 2004 na Sheria ya Usimamizi wa Maafa, Na. 6 ya mwaka 2022 lengo likiwa ni kuendelea kuimarisha masuala ya usimamizi wa maafa.
Amefafanua kuwa,sheria hiyo imebainisha majukumu na imeweka mfumo wa usimamizi wa maafa kupitia Kamati za Usimamizi wa Maafa kutoka ngazi ya Taifa hadi Kijiji/Mtaa.
Amesema,lengo ni kuhakikisha Wizara, Idara, Taasisi za Serikali na zisizo za Serikali, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa zinashiriki kikamilifu katika kutekeleza shughuli za kuzuia na kupunguza madhara ya majanga pamoja na kujiandaa, kukabiliana na kurejesha hali kwa ubora pindi maafa yanapotokea.
Dkt. Yonazi alieleza kwamba ili kuwezesha utekelezaji wa shughuli za usimamizi wa maafa kwa ufanisi, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu kwa kushirikiana na wadau pia imeendelea kuboresha utaratibu wa utekelezaji wa shughuli za usimamizi wa maafa nchini kwa kuandaa nyaraka zinazoainisha majukumu ya msingi kwa wadau na zinazotoa mwongozo wa majukumu kwa wadau.
Aidha,nyaraka hizo ni pamoja na Mpango wa Taifa wa Kujiandaa na kukabiliana na Maafa (2022), Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano Wakati wa Maafa (2022 na Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Maafa (2022).
Dkt.Yonazi amesema, nyaraka ziwe ni chachu ya kuongeza ushirikishwaji wa jamii na wadau pamoja na kupunguza madhara ya majanga na kujiandaa na kukabiliana na maafa,”alieleza Dkt. Yonazi.
“Natambua, kwa sasa halmashauri inaendelea kutekeleza shughuli za kurejesha hali baada ya maafa makubwa yaliyosababishwa na janga la maporomoko ya ardhi katika mlima Hanang yaliyotokea mwaka jana.
"Niendelee kusisitiza kuwa, muendelee kutoa elimu kwa jamii kuhusu namna ya kuzuia na kupunguza madhara ya majanga na kujiandaa na kukabiliana na maafa na kuwahamasisha wananchi kutokutekeleza shughuli za kiuchumi na ujenzi katika maeneo hatarishi kwa kuzingatia ushauri wa kitaalamu,”amesema Dkt.Yonazi.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Hanang’ na Mwenyekiti wa Kamati Elekezi ya Usimamizi wa Maafa ya Wilaya Mhe. Almishi Hazali ameishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuendelea kuratibu maafa nchini, huku akipongeza hatua ya uzinduzi wa nyaraka hizo muhimu katika Wilaya hiyo na kueleza kuwa, ni nyenzo muhimu katika kuendeleza jitihada juu ya majanga na maafa nchini.