Serikali imeendelea kuwekeza kwa kasi katika TEHAMA-Waziri Silaa

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa (Mb) amefungua rasmi Kongamano la Nane la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Tanzania.
Kongamano hilo limeanza Oktoba 13,2024 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (The Julius Nyerere International Convention Centre-JNICC) jijini Dar es Salaam na linatarajiwa kufikia tamati Oktoba 17, 2024.

Amesema, wizara anayoiongoza pamoja na majukumu mengine amepewa jukumu la kusimamia TEHAMA ya mwaka 2016 ambayo imebainisha masuala ya kisera, kisheria na taasisi katika kukuza matumizi ya TEHAMA nchini.

"Katika kutekeleza Sera ya TEHAMA, Serikali kupitia Amri ya Rais ilianzisha Tume ya TEHAMA ambayo ilipewa majukumu ya kusimamia utekelezaji wa Sera ya TEHAMA,kukuza uwekezaji katika TEHAMA, kujenga uwezo na kukuza utaalamu katika fani ya TEHAMA."

Jukumu lingine, Mheshimiwa Waziri Sillaa amesema ni pamoja na Tume ya TEHAMA kushirikiana na wadau wengine katika masuala ya utafiti.

"Utekelezaji wa majukumu niliyoyataja ndiyo yamepelekea uwepo wa kongamano hili ambapo wadau na wataalamu mbalimbali wanapata nafasi ya kujadili masuala mbalimbali yatakayowezesha utekelezaji wa Sera ya TEHAMA nchini.

"Lakini, pia kwenda sawa na mabadiliko ya teknolojia hususani zinazoibukia kama Akili Mnemba, Roboti na Big Data Analytics.Nimejulishwa kuwa, kongamano hili la nane tangu kuanzishwa kwa Tume ya TEHAMA, pia limetanguliwa na mkutano wa wanawake katika TEHAMA pamoja na vijana wana TEHAMA."

Waziri Silaa amesema, kupitia mikutano hiyo miwili ambayo imefanyika Oktoba 13 na 14,2024 masuala mbalimbali yahusuyo TEHAMA yalijadiliwa.

Amesema, kongamano hili ambalo amefungua leo Oktoba 15,2024 lina kauli mbiu isemayo Kutumia Uwezo wa Akili Mnemba na Roboti kwa Mapinduzi ya Kiuchumi na Kijamii.

Waziri Silaa amesema, kauli mbiu hiyo inafungua mjadala muhimu hususani kwa wakati huu ambapo Dunia nzima inashuhudia mapinduzi ya kidigitali.

"Sisi kama Taifa tunayo nafasi ya kutumia teknolojia hizi ili kuboresha ustawi wa wananchi wetu na kuongeza tija katika uchumi."

Vilevile amebainisha kuwa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza kwa kasi kubwa katika TEHAMA ambayo ndiyo nguzo kuu ya kufikia uchumi wa kidigitali.

"Dunia hivi sasa ipo katika kipindi cha mapinduzi ya nne, ya tano na ya sita ya viwanda ambapo shughuli za kiuchumi, kijamii na kiuzalishaji kwa kiasi kikubwa inakwenda kuendeshwa kwa kutumia teknolojia za juu za TEHAMA."

Waziri Silaa amebainisha kuwa, kwa umuhimu huo Serikali imeendelea kuwekeza katika kufanya maboresho ya kisera, kisheria na kitaasisi ikiwemo kujenga uwezo kwa Watanzania ili kuhakikisha Tanzania inakuwa sehemu ya mabadiliko katika masuala ya TEHAMA duniani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news