KILIMANJARO-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali imetenga shilingi bilioni 20.21 kwa ajili ya watu wenye ulemavu ikiwa ni mikopo yenye masharti nafuu na isiyokuwa na riba inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri.
Amesema hayo leo Oktoba 25, 2024 alipomwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Fimbo Nyeupe na Miaka 60 ya Chama cha Wasioona Tanzania (TLB) mkoani Kilimanjaro.
“Katika mwaka wa fedha 2023/2024, Halmashauri zilitenga shilingi bilioni 16.14, hili ni ongezeko kubwa. Viongozi wa vyama vya watu wenye ulemavu wekeni utaratibu ili wanachama wenu waweze kunufaika na fursa hii ambayo Serikali imeitoa kwa watu wenye ulemavu.”
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali kupitia Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Miradi (UNOPS)imewezesha kupatikana ruzuku ya shilingi bilioni 8.2 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kuwapima watoto wasioona na viziwi.
“Wale watakaobainika wanahitaji vifaa saidizi watapewa bila malipo. Mradi huu unaanza kutelezwa mwezi Novemba, 2024 ambapo zaidi ya watoto 300,000 wenye changamoto za uoni watanufaika.”
Waziri Mkuu ameongeza kuwa, kwa mwaka wa fedha 2024/25 Serikali inatarajia kujenga miundombinu fikivu ya elimu vikiwemo vyumba vya madarasa 6,357, matundu ya vyoo 1,482, kumalizia mabwalo 362 na kukamilisha mabweni 36.
“Aidha, Serikali imepanga kujenga shule mpya fikivu 184 na mabweni 186 katika shule za sekondari.”
Akizungumzia kuhusu tabia ya baadhi ya Wazazi na walezi kuwaficha watoto wenye ulemavu, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito wa viongozi wa vyama vya wenye ulemavu kwa kushirikiana na Maafisa Maendeleo ya Jamii kuwenda hadi kwenye ngazi ya vitongozi kuhakikisha watoto wenye ulemavu hawafichwi.
“Hakuna sababu ya kumficha mwenye ulemavu, mtoe na mtambulishe Serikalini ili apate fursa na ashiriki katika huduma za kijamii, ikiwemo afya na elimu, Serikali imefungua milango ya huduma kwa ajili yao.”
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa upatikanaji wa teknolojia saidizi na fikivu ni muhimu ili kuhakikisha watu wenye ulemavu wa kuona wanapata fursa za maendeleo na wanaweza kuchangia kwa ufanisi katika uchumi wa nchi.
Kwa upande wake Katibu wa Chama Cha Wasioona, Bw. Loata Mollel amemshukuru Rais Dkt. Samia kwa kutoa fedha za ruzuku kiasi cha shilingi milioni 16.8 ambazo zimewezesha kugharamia utekelezaji wa kazi za Chama hicho.
“Pia tunaishukuru Serikali kwa uamuzi wa kushirikisha watu wenye ulemavu kwenye maandalizi ya dira ya Taifa ya Maendeleo na tunaamini masuala yetu yatajumuishwa kwenye dira hiyo.”
Ameongeza kuwa Maadhimisho hayo yanakusudia kuitambulisha fimbo nyeupe kwa jamii kuwa ni alama na nyenzo ya usalama na kuonesha uwezo wa wasioona katika kushiriki kwenye masuala mbalimbali ya maendeleo na shughuli za kiuchumi.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Mhandisi Rogatus H. Mativila amesema kuwa TAMISEMI kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa Elimu wameendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia wanafunzi wote wakiwemo wenye mahitaji maalum.
Naye, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Zuhura Yunus amesema kuwa Amesema kuwa Serikali inaendelea na zoezi la kuleta maendeleo na Ustawi kwa Watu wenye Ulemavu wakiwemo Wasiona kwa kuhuisha Sera ya Taifa ya Huduma na Maendeleo kwa Watu wenye Ulemavu ya mwaka 2004.