ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi amebainisha, tayari Serikali imejenga madarasa 2,738 kwa kuvuka lengo la Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020 - 2025 ambayo ilielekeza kujengwa madarasa 1,500.
Amesema,hatua hiyo inakusudia kutekeleza azma ya Serikali ya kuona wanafunzi wanasoma kwa mkondo mmoja chini ya wanafunzi 45 katika darasa moja huku serikali ikiweka mkazo zaidi kwenye masomo ya hisabati na sayansi.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Oktoba 23, 2024 alipofungua Skuli mpya ya Sekondari ya ghorofa tatu, Mkokotoni Mkoa wa Kaskazini Unguja, ikiwa ni mwendelezo wa wiki ya kupongeza juhudi za Serikali ya awamu ya nane kufuatia mafanikio makubwa yaliyopatikana chini ya uongozi wa miaka minne ya Dkt. Mwinyi.
Aidha, Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa uzinduzi wa skuli hiyo ni kuimarisha mifumo na miundombinu ya elimu ili kufanikisha mageuzi makubwa yanayoendana na teknolojia ya sasa ulimwenguni.
Rais Dkt.Mwinyi amesisitiza kuwa hadi sasa Wizara ya Elimu imetengewa bajeti ya shilingi bilioni 830 ambayo inatarajiwa kuongezeka hadi kufikia shilingi Trilioni moja kutoka bajeti ya miaka mitatu nyuma ya bilioni 83.
Rais Dkt.Mwinyi amesema Serikali itaendelea kuongeza bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwani ni sekta ya kipaumbele kwa maendeleo ya nchi.
Halikadhalika Kuhusu maslahi ya walimu Rais Dkt. Mwinyi amesema, Serikali itaendelea kuongeza hasa kwa wanaofanyakazi kwenye mazingira magumu, huku akiwasisistiza vijana kusoma zaidi kwani Serikali yao inaendelea kuwajengea mazingira mazuri.