Serikali imeweka kipaumbele katika maendeleo ya jamii-Rais Dkt.Mwinyi

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema, Serikali imeweka kipaumbele kwenye maendeleo ya jamii endelevu, ikiwemo ujenzi wa nyumba za bei nafuu na kuhakikisha upatikanaji wa huduma muhimu za maji safi, usafi wa mazingira, na umeme.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo katika Hoteli ya Melia, Kiwengwa Mkoa wa Kaskazini Unguja, kwenye mkutano wa mwaka wa pamoja kati ya Umoja wa Afrika na Jumuiya za Taasisi zinazojishughulisha na mikopo ya nyumba kutoka nchi za Umoja wa Afrika (AUHF).
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ameongeza kuwa, Serikali imepiga hatua kubwa za kukabiliana na mahitaji ya makazi ya watu wanaoongezeka siku hadi siku, kwa kuzingatia uwezo wa kumudu gharama za nyumba na makaazi endelevu.
Rais Dkt.Mwinyi amezisihi taasisi hizo kutoa mikopo nafuu ili wananchi waweze kumudu gharama za nyumba kwa urahisi.
Ameeleza kuwa, Serikali kupitia Shirika la Nyumba la Zanzibar (ZHC), imeweka mipango kadhaa ya kuinua upatikanaji wa nyumba za bei nafuu, hasa kwa familia za kipato cha chini na cha kati, ikiwemo ujenzi wa miradi mikubwa ya nyumba inayokidhi mahitaji ya ukuaji wa miji na kuhakikisha Serikali inafanikisha malengo yake.
Halikadhalika, Rais Dkt. Mwinyi ameisifu Kampuni ya TMRC kwa kuboresha upatikanaji wa mikopo ya nyumba nchini Tanzania, kuweka wepesi wa umiliki wa nyumba kwa watu wengi, na kuchochea sekta ya ujenzi, hivyo kuzalisha ajira nyingi na kuchangia ukuaji wa uchumi.
Vilevile, Rais Dkt. Mwinyi amewapongeza wafanyabiashara na taasisi za Kitanzania kwa kupiga hatua kubwa na kuendeleza makazi ya gharama nafuu na maendeleo ya mijini, wakiwemo Watumishi Housing Company (WHC) ambao ni wahusika wakuu katika kushughulikia mahitaji ya makazi ya Watanzania, Benki Kuu ya Tanzania, na CRDB, ambayo inaongoza kwa utoaji wa mikopo ya nyumba kwa wananchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news