ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema, Serikali zote mbili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zinajitahidi kukabiliana na changamoto zilizomo kwenye sekta ya afya nchini.Miongoni mwa hatua amesema ni kupunguza vifo vya mama na mtoto, kuhakikisha upatikanaji wa dawa muhimu, uimarishaji wa miundombinu ya afya, upatikanaji wa taarifa za afya, udhibiti wa maradhi ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza na mengineyo.
Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo Oktoba 3, 2024 wakati alipofunga kongamano la 11 la mkutano wa masuala ya Afya Tanzania, lililoshirikisha mataifa 11 duniani katika viwanja vya Maonesho ya Biashara Dimani, Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Aidha Rais Dkt. Mwinyi, amesisitiza kuwa changamoto zote zilizojadiliwa kwenye kongamano hilo, zinahitaji kuchukuliwa hatua madhubuti na za haraka, na kueleza kuwa Kongamano hilo, sio tu jukwaa la majadiliano, bali pia ni chombo cha kuchochea utekelezaji wa mipango mbalimbali ya kuimarisha afya za wananchi.
Amesema, tathmini ya mkutano huo imeonesha mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta ya afya kupitia ubunifu na matumizi ya teknolojia, kama vile programu za Afya za kidigitali zinazosaidia kuimarisha huduma za afya na mifumo ya taarifa za afya.
Halikadhalika alieleza kuwa ni fursa muhimu kwa wataalamu wa afya, viongozi wa Serikali, na wadau wengine wa Maendeleo kutoka Sekta za Umma na Binafsi kuungana na kubadilishana uzoefu, kuhusu mustakabali wa Sekta ya afya Tanzania na Afrika kwa ujumla.