Serikali inaendelea na ujenzi wa miundombinu bora katika Sekta ya Afya-Rais Dkt.Mwinyi

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea na ujenzi wa miundombinu, ikiwemo hospitali za wilaya na vituo vya afya katika maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba, ili kuhakikisha wananchi wanapata matibabu bora.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 21 Oktoba 2024, alipozungumza na timu ya Madaktari Bingwa kutoka Taasisi ya Umoja wa Madaktari Bingwa wenye asili ya India wanaoishi Marekani (GAPIO) Ikulu, Zanzibar, kuelezea dhamira yao ya kushirikiana na Serikali kuimarisha sekta ya afya katika maeneo mbalimbali.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amebainisha kuwa Zanzibar inahitaji kuungwa mkono zaidi, hasa kwenye maeneo ya utaalamu, miundombinu, na kuwajengea uwezo watendaji wa sekta ya afya ili kutoa huduma bora kwa wananchi.

Akizungumzia kuanzishwa kwa bima ya afya kwa wenyeji na wageni wanaoingia nchini, Dk. Mwinyi amesema kuwa bima hiyo inasaidia kupatikana kwa fedha za uendeshaji wa Sekta ya Afya, akitolea mfano wa watalii 18 ambao wamenufaika na bima hiyo.
Vilevile, ameeleza kuwa Serikali inakusudia kuimarisha huduma za bima ya afya kwa njia ya kidigitali ili kurahisisha wageni kupata huduma hiyo hata wakiwa nje ya Zanzibar.

Halikadhalika, Rais Dkt. Mwinyi ameihakikishia timu ya madaktari hao kuwa Serikali ipo tayari kushirikiana nao kwa kuandaa mazingira rafiki ya kufanya kazi pamoja na mipango ya muda mfupi, wa kati, na mrefu ili kuimarisha ushirikiano baina ya Serikali, kupitia Wizara ya Afya, na taasisi ya GAPIO.
Naye Mratibu wa ujio wa madaktari hao kutoka Hospitali ya Apollo ya Dar es Salaam, Dk. Nazir Arab, amesema kuwa lengo la taasisi yao ni kusambaza madaktari zaidi ya 1.4 milioni duniani, Tanzania ikiwemo Zanzibar, kuwa miongoni mwa nchi zitakazofikiwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news