ARUSHA-Serikali imewahakikishia wananchi kuwa ina dhamira ya dhati ya kutekeleza mpango wa bima ya afya kwa wote, na kutoa wito kwa washiriki wa kongamano la mpango wa bima ya afya kwa wote na mdahalo wa kitaifa kuhusu ufadhili wa sekta ya afya kuja na mapendekezo yatakayosaidia kutimiza dhamira hiyo.
Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) wakati anafungua matukio hayo mawili yanayofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha jijini Arusha Oktoba 30, 2024.
Matukio hayo yanayofanyika kwa siku nne hadi Novemba 1, 2024 yamekusanya wadau wa afya kutoka ndani na nje ya nchi ili kwa pamoja kujadili mikakati na mbinu bora zitakazoiwezesha Serikali kuwa na mipango endelevu ya kuhakikisha kuwa kila mwananchi, anakuwa na bima ya afya itakayomwezesha kupata matibabu bila kuangalia kipato chake.
Waziri Mkuu ambaye aliambatana na viongozi mbalimbali katika hafla hiyo ya ufunguzi, wakiwemo Waziri wa Afya, Mhe. Jenista Mhagama (Mb), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Denis Londo (Mb) na viongozi wa mkoa wa Arusha, amesema kuwa Serikali imejiandaa vyema kutekeleza mpango wa bima ya afya kwa wote kwa kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya.
Imeelezwa kuwa tokea aingie madarakani, Rais Samia Suluhu Hassan, jumla ya trilioni 6.2 zimeelekezwa katika sekta ya afya. Fedha hizo zimetumika kujenga miundombinu kuanzia ngazi ya msingi hadi taifa, ununuzi wa vifaa tiba na kuwapatia ujuzi na elimu watumishi wa sekta ya afya.
Umetolewa mfano kuwa wakati Rais Samia anaingia madarakani, nchi ilikuwa na upungufu wa madaktari bingwa 2989, lakini kwa kipindi cha miaka mitatu tu, kupitia Ufadhili wa Mama Samia (Samia Scholarships), madaktari bingwa 1485 wamesomeshwa na kupunguza upungufu huo kwa takribani nusu.
Mhe. Waziri Mkuu amesema uwepo wa madaktari hao, ujenzi wa hospitali za ngazi mbalimvali pamoja na ununuzi wa vifaa vya kisasa umeiwezesha nchi kuwa na uwezo wa kufanya tiba za kibingwa kama vile upandikizaji wa figo, uboho, mimba na vifaa vya kusikia ambapo awali tiba hizo zilikuwa zinapatikana nje ya nchi.
Eneo lingine ambalo Serikali imeliimaalisha ni upatikanaji wa dawa katika ngazi zote kuanzia zahanati hadi hospitali za rufaa. Imeelezwa kuwa upatikanaji huo unatofautiana ambapo unaanzia asilimia 75 katika zahanati hadi 98 kwa hospitali za rufaa. Bohari Kuu ya Dawa imejenga vituo kila kanda na baadhi ya halimashauri ili kurahisisha usambazaji wa dawa katika maeneo husika.
Waziri Mkuu amesema kuwa uwekezaji katika sekta ya afya umepunguza vifo kwa asilimia 20 hadi 30 na matarajio ni kwamba mpango wa bima ya afya kwa wote utakapokamilika utapunguza zaidi vifo nchini.
Waziri Mkuu alihitimisha hotuba yake kwa kutoa maelekezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Wizara ya Afrya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa bima ya afya kwa wote, ili itakapoanza kusiwe na mtu atakayeachwa nyuma.
Awali, Mhe. Naibu Waziri Londo alisema kuwa kufanyika kwa mdahalo wa kitaifa kuhusu ufadhili wa sekta ya afya ni utekelezaji wa maagizo ya Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Afya la Jumuiya ya Afrika Mashariki, waliyoyatoa wakati wa mkutano wao uliofanyika jijini Dar Es Salaam mwezi Mei 2024. Aidha, ameongeza kuwa mdahalo huo ni mwendelezo wa vita vilivyoasisiwa na waasisi wa taifa hili dhidi ya maadui wakubwa watatu ambao ni maradhi, umasikini na ujinga.
Matukio hayo yamehudhuriwa na wadau wa maendeleo na nchi marafiki kama vile Shirika la Afya Duniani, Mfuko wa Afya, Shirika la Maendeleo la Korea (KOICA), Jamhuri ya Korea, Indonesia, Rwanda ambao wameahidi kuwa watashirikiana na Serikali ya Tanzania katika safari yake ya kufikia bima ya afya kwa kila mwananchi.