ZANZIBAR-Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, imesema itaendelea kukuza mazingira rafiki ya biashara na uwekezaji pamoja na kuweka mkazo wa kurahisisha michakato, kuimarisha mifumo ya udhibiti na kutoa motisha za kuvutia uwekezaji nchini.

Amesema, Zanzibar imefungua milango wazi kwa fursa za biashara na uwekezaji na tayari imewakaribisha wadau mbalimbali kushirikiana nao kwenye maono ya ukuaji wa Uchumi endelevu na ustawi wa utalii wa muda mrefu.
Amesema, maonesho hayo yamedhihirisha thamani ya ushirikiano baina ya wadau wa utalii nchini, Sekta ya Umma na Kibinafsi (PPP) na kueleza kuwa ushirikiano wao ni njia muhimu za kufikia malengo ya pamoja.
Rais Dkt. Mwinyi aliwashauri wadau wa Utalii kuendeleza utamaduni na shauku ya kufanya Maonesho ya Utalii na Uwekezaji si kwa mnasaba wa Zanzibar pekee bali kwa Afrika Mashariki na medani za kimataifa ili kuendelea kuitangaza nchi na vivutio vyake duniani kote.
Amesema, hatua hiyo itaiwezesha Zanzibar kuwa kituo bora cha ushindani kwa utalii kwenye ramani ya dunia.

Ameeleza kuwa maonyesho hayo yanaashiria mwanzo wa mashirikiano mapya na wa kudumu na ubunifu tu sio dhamira ya utalii na uwekezaji peke bali ari ya pamoja ya kuhakikisha kuwa Zanzibar inakuwa kinara wa ukuaji endelevu, uhifadhi wa utamaduni na maendeleo ya kiuchumi.
Katika hatua nyingine Rais Dkt. Mwinyi amesema Sekta ya utalii licha ya kuwa ni utii wa mgongo wa pato la Uchumi wa nchi lakini, inaakisi nadharia nzima ya maisha ya Wazanzibari, elimu kwa vizazi vilivyopo pamoja na kuhifadhi utamaduni wa utambulisho wa taifa.
Dkt. Mwinyi amebainisha kwamba, faida za utalii na uwekezaji zinufaishe visiwa vyote vya Unguja na Pemba kwa kutengeneza fursa kwa watu wote.
Akizungumza kwenye maonesho hayo, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudrick Ramadhan Soraga amepongeza juhudi za Maendeleo zinazofanywa na Rais Dk. Mwinyi na kueleza kuwa mafanikio makubwa yaliyopo kwenye sekta ya Utalii ni kazi kubwa inayofanywa Dkt. Mwinyi.
Aidha, amelielezea miaka minne ya mafaniko kwenye uongozi wa Dkt. Mwinyi imeakisi maendeleo enedelevu ya Sekta ya utalii na kukuza biashara na uwekezaji nchini.
Maonesho hayo ya Utalii na uwekezaji Zanzibar, 2024 yameandaliwa kwa ushirikiano na Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale, Kamisheni ya Utalii, na sekta binafsi.
