ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapindizi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewahakikishia wananchi kwamba Serikali itaendeleza ujenzi wa miundombinu ya barabara nchi nzima na kuwasisistiza kuunga mkono juhudi hizo.
Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo alipofungua barabara mpya ya Jozani, Charawe, Ukongoroni hadi Bwejuu, Mkoa wa Kusini Unguja yenye urefu wa kilomita 24.5.
Aidha,Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa wananchi wanawajibu mkubwa wa kutunza barabara zinazojengwa katika maeneo yao, kuonesha kuthamini juhudi kubwa zinazochukuliwa na Serikali kuwajengea miundombinu bora ya usafiri na kuwaondoshea usumbufu waliokuwa wakiupata siku za nyuma.
Rais Dkt. Mwinyi amewathibitishia wananchi wa Mkoa wa Kusini Unguja kuwamalizia barabara ya Tunguu - Makunduchi kwa kiwango cha njia nne zenye taa kutoka Mwanakwerekwe hadi Makunduchi.
Halikadhalika Rais Dkt. Mwinyi, amesema tayari Serikali imejenga skim nne kuu za maji safi ambazo zitamaliza tatizo la maji mkoani humo.
Vilevile Rais Dkt. Mwinyi ameridhia ombi la Wananchi wa Kusini la kujengewa daraja lililoombwa na wananchi wa mkoa huo, litalounganisha Mkoa huko na wa Kaskazini Unguja lengo ni kurahisisha Mawasiliano baina ya mikoa miwili hiyo na huduma nyengine za uchumi na jamii.
Kwa upande mwingine Rais Dkt.Mwinyi ameiagiza Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi kusimamia hifadhi za barabara na kuwazuia wananchi kutojenga na kufanya biashara maeneo hayo ili kukwepa mzigo mkubwa wa fidia kwa Serikali pale inapotaka kupitisha miundombinu mengine muhimu.