Serikali itasimamia kikamilifu utaratibu wa Hijja-Rais Dkt.Mwinyi

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema, Serikali inajipanga vema kusimamia kikamilifu utaratibu wa Hijja kuondokana na changamoto zinazojitokeza wakati wa utekelezaji wa ibada hiyo nchini Saudi Arabia.
Rais Alhaj Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Oktoba 5, 2024, Viwanja vya Ikulu, Zanzibar kwenye Mkutano wa Tathmini ya Ibada ya Hijja iliyopita uliowajumuisha watendaji wa taasisi za Hijja nchini.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amezitaka Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Zanzibar na Baraza la Waislam Tanzania BAKWATA kuwa na Udhibiti imara kwa taasisi zinazosafirisha Mahujaji.

Halikadhalika Rais Dkt.Mwinyi ametoa rai kwa taasisi hizo kujitathmini na kuwa na udhibiti wa taasisi hizo ili kuifanya Ibada ya Hijja kuwa na mazingira bora kwa Mahujaji.

Amefahamisha, ni vyema kuwa na vikao vya pamoja baina ya BAKWATA, taasisi zinazosafirisha mahojaji na Kamisheni ya waqfu na Mali ya Amana, Zanzibar kwa lengo la kuzipatia ufumbuzi wa mapema changamoto zinazojitokeza wakati wa hijja.
Vilevile Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza uadilifu kwa taasisi za Hijja kwa kuwaambia ukweli Mahujaji na kuwapatia taarifa sahihi juu ya Ibada hiyo ili kujiandaa vyema.

Kwa upande mwingine, Rais Alhaj Dkt.Mwinyi amesema Serikali itatoa kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 12 kuziba pengo la Ukosefu wa fedha za kigeni linalojitokeza wakati wa kuwasafirisha Mahujaji kipindi cha utekelezaji wa Ibada ya Hijja.
Amesisitiza kuwa, Serikali itakuwa sehemu ya utatuzi wa changamoto za Hijja.
Rais Alhaj Dkt. Mwinyi amethibitisha kuwa Serikali itaharakisha suala la kuanzishwa kwa Mfuko wa Hijja hapa nchini, utakaosimamia kwa ufanisi masuala ya Hijja.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news