NA LUSUNGU HELELA
Dodoma
SERIKALI imesema itaendelea kuchukua hatua dhidi ya watumishi wa umma wanaothibitika kukiuka maadili ya utumishi wa umma huku ikiahidi kuwekeza zaidi katika matumizi ya TEHAMA ili kudhibiti vitendo vya ukiukwaji wa Maadili. Katibu Mkuu, UTUMISHI, Bw.Juma Mkomi ametoa kauli hiyo leo jijini Dodoma wakati akifunga Kikao kazi cha kubadilishana uzoefu wa masuala ya Maadili na Utawala Bora baina ya Taasisi Simamizi za Maadili ya Utendaji na Mamlaka Simamizi za Maadili ya Kitaaluma.
Amesema,Serikali haitawafumbia macho watumishi wala rushwa na walevi na wenye tabia na mienendo isiyofaa kwenye jamii.
‘’Hivi karibuni nimewahamisha watumishi wanne kutoka wizara fulani wanaotuhumiwa kushiriki mapenzi ya jinsia moja na kuna baadhi ya watumishi wanalala baa na asubuhi wanakwenda kazini wakiwa wachovu na hawajapiga mswaki na hivyo kuwapa shida wananchi wanapowahudumia,’’ ameng’aka Katibu Mkuu Mkomi.
Amesema, dhana ya utumishi wa umma ni maadili na bila maadili hakuna utumishi wa umma hivyo Serikali itaendelea kufanya tahtmini kwa kina kuhusu tabia na mienendo ya watumishi wa umma wakati wote.