ZANZIBAR-Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inalenga kuendeleza zoezi la ugawaji wa boti za uvuvi kwa kila Mkoa wa Unguja na Pemba ili kuisaidia jamii kujiwezesha kiuchumi.
Hayo yamezungumzwa na Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Mhe. Shaaban Ali Othman wakati wa Uzinduzi wa Kampeni ya awamu ya pili ya Mkono kwa Mkono iliyofanyika Madinat Al Bahari, Mbweni Zanzibar.
Amesema, jumla ya boti 10 zitatolewa ambapo kila mkoa utapatiwa boti mbili ikiwemo ya uvuvi na ukulima wa mwani kuisaidia jamii kujikwamua na hali ngumu ya maisha.
Amewataka wadau mbalimbali na wenye dhamana kutoa uelewa kwa wananchi juu ya fursa za kiuchumi zilizopo nchini ili wapate uelewa wa fursa hizo na kuzifanyia kazi.
Naye Mkurugenzi wa Wakala wa Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA), Juma Burhani amesema, taasisi hiyo kwa kushirikiana na vyuo vikuu wanatarajia kuwawezesha vijana 15 hadi 20 kwa kuwapatia mafunzo ya ujasiriamali ili kuwainua vijana hao kiuchumi katika kujiajiri na kuajiri wengine.
Amesema, kupitia kampeni hiyo wanategemea kuvipitia na kuvitambua viwanda mbalimbali vya Unguja na Pemba na kuwashajihisha wananchi kuvitumia viwanda hivyo.
“Mkono kwa Mkono wa msimu uliopita imewasaidia wananchi kupata mikopo baada ya kueleza changamoto zao,” alisema Mkurugenzi Burhan.
Kwa upanda wao Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) wamesema wataendelea kutoa taarifa na kuzisambaza kwa wananchi ili kuelewa miradi mbali mbali inayotekelezwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Kampeni ya Mkono kwa Mkono itaanzia Mkoa wa Kusini Unguja katika Ukumbi wa Dkt. Shein Tunguu siku ya Jumamosi Oktoba 19, 2024.