MTWARA-Serikali imesema iwe jua ama mvua itajenga Kongani ya Viwanda vya kuchakata mazao ya mikoa ya kusini kwa gharama ya zaidi ya sh. Bilioni 300.
Akizungumza katika mwendelezo wa ziara yake mkoani Mtwara Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe (Mb) amesema iwe jua ama mvua itajenga Kongani ya viwanda vya kuchakata mazao ya mikoa ya kusini eneo la Maranje mkoani Mtwara yenye gharama ya zaidi ya sh. Bilioni 300.
Kongani ya Viwanda(Industrial Park) inajengwa katika kijiji cha Maranje na Tulia,kata ya Mtiniko Nanyamba Mji, Mkoani Mtwara
Amesema eneo la mradi lina jumla ya ekari 1,572,ambapo eneo linaendelezwa kwa sasa ni ekari 354 na ekari 1,218 zilizobaki zitasafishwa na kuwekewa fensi mwezi ujao.
Waziri Bashe ameeleza kuwa, Kongani hiyo ya viwanda ndio suluhisho la changamoto walizonazo wakulima wa mikoa hiyo.
“Wapo watu walisema ni ndoto haitawezekana leo nawaambia Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ni msikivu na mtendaji, ameamua iwe jua iwe mvua kongani itajengwa hapa na itahusisha viwanda mbali mbali vya kuchakata korosho, ufuta, mbaazi na mengine,”amesema Waziri Bashe
Amesema Serikali imeanza hatua za awali za ujenzi wa kongani hiyo na zaidi ya sh. Bilioni 7 zimewekezwa.
“Mradi huu mkubwa unaoitwa Dkt.Samia Suluhu Hassan, unalenga kujenga viwanda vya kubangua korosho visivyopungua 30 kwa awamu na tayari zaidi ya shilingi bilioni 7 zimetumika kujenga maghala mawili na kisima kimoja,”amesema Bashe.
Ameongeza kuwa maghala hayo mawili ya awali, yenye uwezo wa kuhifadhi tani 20,000 za korosho, yanatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba mwaka huu, ili msimu wa korosho wa mwaka kesho uanze kwa ufanisi.
Amesema, mradi huo pia utatoa fursa za ajira kati ya watu 33,000 mpaka 35,000 ambapo ajira za kwanza zitanufaisha wananchi wenyeji.
“Mradi huu unatarajiwa kuajiri kati ya watu 33,000 mpaka watu 35,000 na utakuwa suluhisho la changamoto ya muda mrefu juu ya bei ya korosho kwa mikoa yote inayolima korosho ikiwemo Mtwara, Ruvuma, na Lindi, serikali yenu ni sikivu haitarudi nyuma hiki kiwanda kitajengwa kwa maslahi ya wananchi wa kusini,”amesisitiza Bashe.
Aidha Waziri Bashe, amemshukuru Rais Samia kwa kuridhia kurejeshwa kwa agenda ya ushuru wa mauzo ya nje lengo ni kuwezesha upatikanaji wa ruzuku na pembejeo ili kumuinua Mkulima.
Bashe amesema kuwa,fedha hizo za ushuru huo zikikusanywa zinarudi Bodi ya Korosho ili kusimamia mahitaji ya korosho.
"Faida zake ni kubwa kwa kuwa ushuru huu sasa unarudi bodi ya Korosho na kuwezesha wakulima wa zao hilo, sasa tumetoka kuzalisha tani 180,000 hadi tani 310,000 na tunatarajia kufikia tani 500,000,”amesema.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Nanyamba Abdallah Chikota amempongeza Waziri Bashe kwa mapambano ya kutetea maslahi ya wakulima wadogo nchini.
“Tunajua mapambano na vita uliyonayo baada ya kuamua kusaidia wakulima wadogo, usirudi nyuma juhudi zako zitalipwa na Mungu sisi wakulima wa korosho Mtwara tunafaidika na hizi ruzuku za pembejeo na kupanda kwa bei,”amesema mhe Chikota.