PWANI-Wizara ya Kilimo imekubali kulipa shilingi bilioni 16 ili kuliokoa shamba la Ushirika Chauru ambalo ni la wakulima wadogo wa Umwagiliaji huko Ruvu Mkoa wa Pwani. Hayo yamebainika katika muendelezo wa ziara za Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe mkoani humo wakati akikagua maendeleo ya chama cha ushirika cha wakulima wa kilimo cha umwagiliaji Ruvu, Chauru Limited 2000 na kuzungumza na wakulima.
“Shamba hili litapimwa kwa ushirikiano kati ya wizara na wilaya na mipaka yake itatambuliwa na kuwekwa alama za TANROAD,”amesema Waziri Bashe.
Bashe amesema kuwa, Wizara ya Kilimo italipa fedha hizo zaidi ya shilingi bilioni 16 na kuweka makubaliano maalum na wakulima ili waendelee kutumia shamba hilo.
“Katika kata hii wakulima wanalima hekta 1800, sawa na zaidi ya hekari 2500,hivyo Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) itatangaza tenda kwa ajili ya uwekaji wa miundombinu ya umwagiliaji na uzio ili wafugaji wasiingie ndani ya mashamba na wakulima walime kwa uhuru."
Aidha, Serikali pia imetoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara na mtambo wa kuchakata mpunga.
Waziri Bashe amesisitiza kuwa,wakulima wa Chauru ni moja ya skimu ambazo hazilipi ada ya Umwagiliaji IDF, hivyo wakati msimu mpya unapoanza, wakulima watalipa ada hiyo ili wawe na sifa ya kupata fedha kutoka hazina.
Pia, Benki ya Kilimo (TADB) itafanya Mkopo wa Vikundi (group financing) kwa wanachama wa Chauru ili wakulima waweze kusaidika na watalipa kwa miaka mitatu kutokana na mapato yao.
Amesema kuwa,Serikali imeendelea kutoa ruzuku kwa wakulima na kutangaza miradi ya umwagiliaji kwa Mkoa wa Pwani, ikiwemo ujenzi wa mabwawa na skimu katika bonde la Ruvu.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge, ameeleza kuwa Mkoa huo unakwenda kuwa kinara wa uzalishaji wa ndizi na chikichi barani Afrika.
Amesema, kilimo cha umwagiliaji kinapata msaada mkubwa kutoka kwa serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, lengo ni kufikia shabaha ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kulisha Afrika na Dunia.
Pia,Waziri Bashe, amehudhuria uzinduzi wa kiwanda cha viuatilifu hai cha Tanzania Biotech Products Limited (TBPL) kilichopo Kibaha, Mkoa wa Pwani. Bashe alisifu kiwanda hicho kwa kutengeneza viuatilifu rafiki kwa mazingira ambavyo vinaweza kuua viwavi jeshi, ambao wamekuwa tishio kwa sekta ya kilimo nchini.
Amesisitiza, umuhimu wa kutumia viuatilifu hivyo na kumuelekeza Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mazao kuhakikisha fedha zinazotengwa kwa ajili ya viuatilifu zinatumika kununua bidhaa za TBPL na kuwafundisha wakulima jinsi ya kuvitumia.