Serikali yaendelea kuchukua hatua mambo yanayokwamisha kodi

DODOMA- Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali dhidi ya mambo yanayokwamisha makusanyo ya kodi, kwa kutoa elimu ya kodi na kuboresha mfumo wa kodi ili kuhakikisha viwango vya kodi vinawiana na hali halisi ya biashara pamoja na kuwahamasisha ulipaji kodi wa hiari.
Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Maida Hamadi Abdallah, aliyetaka kujua mkakati wa Serikali kumaliza tatizo la wafanyabiashara kukwepa kulipa kodi nchini.

Mhe. Chande alisema kuwa, Serikali inaendesha kampeni za uelimishaji ili kuwawezesha wafanyabiashara kuelewa umuhimu wa kulipa kodi na mchango wake katika maendeleo ya Taifa ambapo elimu hiyo hutolewa kupitia njia mbalimbali zikiwemo semina, redio, televisheni, elimu ya mlango kwa mlango, mikutano ya wadau (Stakeholders Forums), pamoja na mitandao ya kijamii.

Aliongeza kuwa Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), imekuwa ikijikita kwenye matumizi ya teknolojia za kisasa ili kuboresha ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha ulipaji kodi unafanyika kwa uwazi na usahihi.

“Matumizi ya TEHAMA katika mifumo ya kodi yameimarisha uwajibikaji, uwazi, na kuongeza ufanisi wa TRA katika ukusanyaji wa mapato. Hii imepunguza ukwepaji kodi, kuimarisha nidhamu ya walipa kodi, na kurahisisha shughuli za biashara nchini”, alibainisha Mhe. Chande.

Alisema licha ya kuendesha kampeni za uelimishaji na kuimarisha mifumo ya kodi, Serikali ilifanya maboresho ya sheria za kodi dhidi ya wafanyabiashara na wananchi wanaokwepa kodi ili kuhakikisha wanalipa kodi na kuongeza mapato ya nchi.

“Sheria za kodi zimeimarishwa ili kuhakikisha kuwa hatua kali zinachukuliwa dhidi ya wale wanaokwepa kodi. Adhabu hizi ni pamoja na faini kubwa, kufungwa kwa biashara, au kufunguliwa mashtaka ya jinai kwa wafanyabiashara watakaobainika kukwepa kodi”, alisema Mhe. Chande.

Vile vile, Mhe. Chande amezishauri Taasisi nunuzi nchnin kutumia mfumo wa NeST na kuchagua njia ya ununuzi inayoendana na thamani ya mradi ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi hasa hasa yenye thamani chini ya shilingi millioni 100.

Alitoa ushauri huo wakati akijibu swali la Mbunge wa Malinyi, Mhe. Antipas Zeno Ngusi, aliyetaka kujua kama Serikali inaona umuhimu wa kuondoa miradi chini ya shilingi milioni 100 katika Mfumo wa NeST ili kupunguza ucheleweshaji.

Mhe. Chande alisema kuwa, Mfumo wa NeST umerahisisha masuala ya ununuzi wa umma na unawezesha matumizi ya njia ya ununuzi wa thamani ndogo usiotumia fedha taslimu kwa kazi za ujenzi hadi zenye thamani ya shilingi millioni 100 ambapo kupitia njia hii Taasisi nunuzi inaweza kununua moja kwa moja kutoka kwa muuzaji wa bidhaa, mkandarasi au mtoa huduma bila ya kuhitaji kuwashindanisha wazabuni zaidi ya mmoja.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news