NA GODFREY NNKO
Zanzibar
KATIKA sekta ya bima nchini, hatua kadhaa zimechukuliwa na Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) ili kupanua wigo wa huduma za bima.
Pia, sekta ya bima imeshuhudia ukuaji endelevu wa mauzo ghafi ya bima ya wastani wa asilimia 15 kwa mwaka kwa miaka mitano iliyopita, ikiashiria kuongezeka kwa uelewa wa umma na kupanuka kwa soko.
Hayo yameyasema leo Oktoba 1,2024 na Waziri wa Fedha, Dkt.Mwigulu Nchemba kupitia hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa 47 wa Mwaka wa Kamati ya Mamlaka za Usimamizi wa Bima,Masoko ya Mitaji na Huduma za Fedha zisizo za Kibenki (CISNA) jijini Zanzibar.
Hotuba ambayo imesomwa kwa niaba yake na Mheshimiwa Ali Suleiman Ameir, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu Zanzibar. Wenyeji wa mkutano huo hapa nchini ni Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) wakishirikiana na Sekretarieti ya CISNA .
Amesema,kuanzishwa kwa bima za wananchi wa kipato cha chini kumepanua wigo wa huduma za bima.
"Aidha, ushirikiano kati ya benki na kampuni za bima katika kutoa huduma za bima (Bancassurance) umeongeza upatikanaji wa bidhaa za bima nchini.
"Utumiaji wa bidhaa za bima umeongezeka kwa kiasi kikubwa hadi asilimia 2.1 mwaka 2023 kutoka chini ya asilimia 1.0 miaka mitano iliyopita."
Waziri Dkt.Nchemba amesema,matumizi ya mifumo ya simu za mkononi kwa malipo ya ada na madai umeongeza upatikanaji wa bidhaa za bima, hasusani katika maeneo ya pembezoni.
Hatua nyingine kubwa iliyofikiwa katika sekta ya bima, Waziri Dkt.Nchemba amesema ni kutungwa kwa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ya 2023.
Amesema, lengo kuu la sheria hii ni kufikisha huduma bora za afya kwa Watanzania wote, bila kujali hadhi yao ya kiuchumi.
"Kwa kutumia njia za usambazaji zinazotumia teknolojia, idadi ya watumiaji wa bima imeongezeka kutoka milioni 13.8 mwaka 2022 hadi milioni 23.5 mwaka 2023."
Aidha, kupitia Umoja wa Bima za Kilimo Tanzania (TAIC), Waziri Dkt.Nchemba amesema, zaidi ya kampuni 15 za bima zinatoa bima za kilimo.
"Kwa kuzingatia vihatarishi vinavyoikabili sekta ya kilimo na umuhimu wa sekta hii katika maendeleo ya kiuchumi, upatikanaji wa bima ya kilimo unatarajiwa kuwa chombo muhimu katika ukuaji wa uchumi na ustawi wa kanda yetu."
Mbali na hayo, Mheshimiwa Waziri Dkt.Nchemba amewaeleza washiriki wa mkutano huo kuwa, ni matarajio yake mkutano huo utaleta matokeo chanya kwa maendeleo ya sekta ya fedha katika Ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
"Ni mategemeo yangu kwamba mijadala yenu itatoa mapendekezo thabiti kuhusu sera, sheria na udhibiti wa maeneo mapya katika sekta ya fedha kama vile taratibu za udhibiti wa Teknolojia za Fedha (FinTechs)."
Jambo lingine, Mheshimiwa Waziri Dkt.Nchemba amesema, ni udhibiti wa mali na watoa huduma za kidijiti (virtual assets and virtual asset service providers) ikiwemo utekelezaji wa malengo ya huduma za bima kwa wote na uratibu wa shughuli za fedha kati ya nchi na nchi.
Amesema, juhudi za ushirikiano zitaendelea kuwa muhimu katika kukabiliana na masuala hayo na mengine yanayoibuka ili kutimiza maono ya pamoja ya kubadilisha masoko ya SADC kuwa eneo la kiuchumi lenye nguvu na linayovutia uwekezaji wa ndani na wa kimataifa kwa maendeleo endelevu.
"Sambamba na hilo, ni muhimu kuendeleza rasilimali ya msingi zaidi yaani watu wetu. Ninawapongeza CISNA kwa kutambua hilo na kuweka sehemu ya mkutano kutumika kwa kujenga uwezo.
"Napenda kurejea ahadi ya Serikali zetu mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuendelea kushirikiana na CISNA na wanachama wake kuweka mazingira wezeshi kwa maendeleo ya huduma za fedha zisizo za benki na uwekezaji kwa ustawi wa kanda yetu na Afrika kwa ujumla."
Mkutano wa 47 wa Mwaka wa Kamati ya Mamlaka za Usimamizi wa Bima, Masoko ya Mitaji na Huduma za Fedha zisizo za Kibenki (CISNA) ambao umefunguliwa leo Oktoba 1, 2024 umeanza Septemba 29,2024 na unatarajiwa kufikia tamati Oktoba 4,2024 jijini Zanzibar.