DAR-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka watumishi wa halmashauri nchini kuendelea kuweka mikakati ya kushirikisha sekta binafsi katika mipango ya kimaendeleo.
Amesema kuwa,kwa kufanya hivyo kutasaidia kuongeza wigo wa utoaji huduma kwa wananchi na uzalishaji wa bidhaa ikiwemo za kwenye sekta ya mifugo.
Amesema hayo leo Jumapili, Oktoba 6, 2024 wakati alipozungumza na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni, jijini Dar es Salaam kwenye ukumbi wa chuo cha Maendeleo ya Wananchi. Waziri Mkuu yupo mkoani Dar es Salaam kwa ziara ya kikazi ya siku mbili.
“Sera yetu ndani ya Serikali inahamasisha sekta binafsi kuwekeza na kutoa huduma, katika idara yako ni lazima ujiulize sekta binafsi imechangia kiasi gani katika kutoa huduma.”
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amewataka madiwani kwenye halmashauri zote nchini kushiriki katika kufanya makadirio ya makusanyo kwenye halmashauri zao kwa kushirikiana na watendaji wa Halmashauri, Kata na Vijiji.
“Baraza la Madiwani kafanyeni Survey ili mzitambue vyanzo vyote na mjue vinachangia kiasi gani, nendeni mkajifunze Temeke namna walivyofanya walivyopandisha makusanyo kutoka milioni 8 kwa wiki mpaka milioni 120”.