SIKU YA MAKAZI DUNIANI:VIJANA WASHIRIKISHWE KUJENGA TASWIRA YA MIJI

NA MUNIR SHEMWETA

TANZANIA inaungana na mataifa yote kuadhimisha Siku ya Makazi Duniani ambayo huadhimishwa Jumatatu ya kwanza ya mwezi wa 10 kila mwaka ambapo mwaka huu inaadhimishwa tarehe 07 Oktoba 2024.
Chimbuko la maadhimisho haya ni Azimio Na. 40/202 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa la mwaka 1985 ambalo nchi wanachama ikiwepo Tanzania ziliazimia kwa kauli moja kuwa kila Jumatatu ya kwanza ya mwezi Oktoba kila mwaka itakuwa ni siku maalum ya kuadhimisha Siku Makazi Duniani.

Maadhimisho ya siku hii hulenga kuwakumbusha watu kuwa, kila mmoja ana wajibu wa kushiriki katika jitihada za kufanya majiji na miji ya badae kuwa bora zaidi.

Hatua hiyo inayafanya maadhimisho ya Siku ya Makazi Duniani kwa kila mwaka huongozwa na kaulimbiu mahususi ambayo hutoa dhamira ya maadhimisho ya mwaka huo.

Kwa kuzingatia hilo, mwaka huu maadhimisho hayo yanaongozwa na kaulimbiu inayosema; “Ushirikishwaji wa Vijana kwa Miji Bora ya baadae na kuwezesha Kizazi kijacho kujenga taswira ya Miji na Jamii wanayoishi” ili kusaidia kutafakari kwa pamoja namna ya kuboresha miji na makazi kwa kuwashirikisha vijana.

Kwa upande wa Tanzania, tunaadhimisha siku hii huku takwimu za jumla zikibainisha kuwepo kwa upungufu wa nyumba za makazi takribani milioni 3 kutokana na kasi kubwa ya ongezeko la idadi ya watu nchini, pengo ambalo linalotokana na upungufu wa nyumba takribani 390,000 kila mwaka.

Athari za upungufu huo zimegusa pia majiji na mijini inayochipukia, ambapo takwimu za makadirio ya upungufu wa mahitaji ya nyumba mijini zinaonesha kuwa kwa mwaka 2022 pekee yalikuwa ni 2,691,441 na inakisiwa ifikapo 2052 upungufu huo utaongezeka na kufikia 19,618,879 sawa na ongezeko la asilimia 629, hivyo kuhitaji mipango thabiti shirikishi yenye mtazamo wa kuwa na maendeleo endelevu ya ukuaji wa miji na makazi kwa ajili ya kujianda kukabiliana na changamoto zitokanazo na ongezeko hilo.

Moja ya changamoto kubwa tunayokabiliana nayo katika kufikia lengo la kuwa na miji endelevu ya baadae kama nchi ni kasi kubwa ya ukuaji wa makazi ya vitovu vya vijiji inayoambatana na vijiji hivyo kuendelea kupoteza hadhi yake ya kuwa vijjiji kwa kusongwa au kumezwa na tabia za kimji kwa namna au ukuaji usioendelevu.

Hali hii inatokana na usimamizi na uratibu duni wa upangaji makazi na ujenzi wa nyumba bora vijijini katika hatua hiyo ya awali ya ukuaji wake kwa mtazamo wa kuviandaa vijiji hivyo kuwa miji endelevu ya baadae na yenye tija kiuchumi na kijamii kwa kizazi kijacho.

Kwa kuzingatia changamoto hiyo Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi tayari imeandaa Mwongozo rahisi wa Upangaji Makazi na Ujenzi wa Nyumba Vijijini wenye lengo la kuwasaidia wakazi wa maeneo husika kupanga makazi ya vijiji vyao na kujenga nyumba bora na za gharama nafuu kwa njia shirikishi kati ya wataalam wa Mipangomiji, wanavijiji na wadau wengine mbalimbali.

Aidha, kupitia pia programu ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha (KKK), kati ya kipindi cha 2018 hadi 2024, Wizara imewezesha upangaji na upimaji wa viwanja 538,429 katika halmashauri 142 ambazo zimejengewa uwezo kwa kukopeshwa fedha kiasi cha Tshs.bilioni 68.8.

Upimaji wa viwanja hivyo umetoa fursa kwa wananchi wengi kupata viwanja kwa shughuli za makazi na fursa za biashara ikiwepo na kundi la vijana na jumla ya mashamba 555 yamepimwa kuiwezesha jamii kiuchumi kupita shughuli za kilimo na ufugaji.

Pamoja na kuadhimisha siku hii ya Makazi Duniani, ulimwengu unakabiliwa na changamoto kubwa ya mabadiliko ya tabia nchi na janga la uharibifu wa mazingira unaotokana na kasi ya ukuaji wa miji kufuatia ongezeko kubwa la idadi ya watu na shughuli za binadamu.

Shirika la Makazi Duniani (UN- HABITAT) kwa kushirikiana na Jumuiya nyingine za kimataifa wanahimiza kuweka mazingira wezeshi ya vijana kuwa wabunifu kwenye masuala ya mabadiliko ya tabia nchi sambamba na kuwajengea uwezo kwa kuwapatia maarifa kuhusu maendeleo endelevu katika kutunza mazingira ya miji na vijiji ili waweze kukabiliana na changamoto hizo ikiwepo na kuwekeza katika sera za ubunifu katika utunzaji mazingira na uendelezaji wa miji endelevu yenye kuchochea ukuaji wa uchumi.

Serikali, chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan imeliona suala hilo na inaendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kujenga uchumi imara na jumuishi wenye kuhusisha makundi yote ya kijamii likiwemo kundi la vijana.

Serikali imefanya imeandaa Sera, Sheria na imeweka mipango mbalimbali jumuishi yenye kuzingatia uwepo wa makundi hayo ya kijamii ili kuwajumuisha na kuelezea katika Sekta ya Nyumba na Makazi.

‘’Kundi hili la vijana mwenye umri wa miaka 15-35 ni sehemu ya makundi makubwa ya jamii nchini Tanzania, nitoe wito kwa wadau mbalimbali kuendelea kushirikiana na serikali kuwashirisha vijana kwenye mipango ya maendeleo ya kisekta pamoja na kuzingatia msisitizo wa Sera katika maeneo yaliyoainishwa kwa kuwahusisha vijana kikamilifu,’’amesema Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Mhe. Deogratius Ndejembi.

Kutokana na vijana wengi nchini ni vyema wadau shiriki wakajikita kutoa elimu kwa vijana ili kuwajengea uwezo na kushiriki kikamilifu katika usimamizi mazingira na uendelezaji wa miji na makazi bora kwa ujumla.

Aidha, kwa kuwa miji midogo na miji mikubwa nchini ni vitovu vya shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii, Vijana wanahamasishwa kuwa wabunifu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kubuni miradi inayotunza mazingira kuanzia ngazi ya kaya hadi miji yetu kwa ujumla.

“Bado ipo haja kubwa ya vijana kushiriki kikamilifu katika upangaji wa miji na kuona umuhimu wa kuendelea kuiboresha miji ili kuhakikisha athari za mabadiliko ya tabia nchi zinakabiliwa,’’ amesema Waziri Ndejembi katika wito wake wa Maadhimisho ya Siku ya Makazi Duniani.

Mwandishi wa Makala hii ni Afisa Habari Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news