DAR-Viongozi na watumishi wa Idara ya Ununuzi na Ugavi ya Hospitali ya Taifa Muhimbili wamepatiwa mafunzo ya kuwakumbusha kuhusu kuzuia na kupambana na rushwa mahala pa kazi.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo Oktoba Mosi,2024, Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi, amesema lengo la mafunzo hayo ni kukumbushana wajibu kama wafanyakazi ambao pia ni watendaji na wawakilishi wa Serikali hospitalini hapo.
“Hii ndio timu inayoendesha hospitali vilevile miradi tuliyonayo ni mikubwa hivyo ni jambo jema kukubushwa wajibu wetu sisi tuliopewa dhamana ya kusimamia hospitali hii,” amesema Prof. Janabi.
Amesema, rushwa ina tafsiri pana, kwani hata kuchelewesha mchakato wa manunuzi ni viashiria mojawapo, hivyo tunaahidi kuwa tutaendelea kutoa mafunzo haya kwa kila kurugenzi ili kuwafikia wafanyakazi wote kuwa na ufahamu.
Kwa upande wao, Afisa Muelimishaji kutoka TAKUKURU Ilala, Bi. Marcella Salu amesema ni muhimu kufahamu kuwa mapambano dhidi ya rushwa si jukumu la Serikali au TAKUKURU pekee bali ni la kila mmoja.
“TAKUKURU ni kama nahodha anayeongoza, lakini nyuma yetu ipo jamii ikiwa ni pamoja na watumishi wa MNH na viongozi kwa ujumla wake ili kushirikiana katika mapambano dhidi ya rushwa hasa katika idara za manunuzi,” amesema Bi. Salu.
Naye Bi. Nerry Mwakyusa ambaye pia ni Afisa Muelimishaji kutoka TAKUKURU Ilala amewashauri watumishi kuzingatia sheria na kanuni zote zilizowekwa katika utekelezaji wa majukumu yao ya kazi ili kutoa huduma bora kwa jamii na kwa haki.
Bi. Mwakyusa ameongeza, ni muhimu kuwa na utaratibu wa ukaguzi wa ndani katika taasisi kupitia kazi zote zinazofanywa ikiwa ni pamoja na kutoa maoni ambayo yatasaidia kubaini viashiria vya rushwa mapema ili kuzuia changamoto za awali.
“Ili kukabiliana na kupambana na rushwa ni muhimu watumishi kuwa wawazi katika uwajibikaji kwa kuandaa nyaraka zote za utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku pamoja na kutotegemea mishahara bali waweze kubuni miradi binafsi ya kujiongezea kipato ili kuepukana na rushwa,”amesema Bi. Mwakyusa.
Tags
Afya
Habari
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
TAKUKURU Tanzania