Tanzania imejiandaa kurusha satelite-Waziri Mkuu

DAR-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa,Serikali inaendelea kutekeleza wa Mpango mkakati wa miaka mitano 2024/25 – 2029/30 wa anga za juu utakaoiwezesha Tanzania kurusha satelaiti.
Amesema kuwa,Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam imepata mradi wa utafiti wa kuwezesha urushaji wa satelaiti unaosimamiwa na Taasisi ya Umoja wa Mataifa ya Masuala ya Anga za Juu ikishirikiana na Taasisi ya Anga za Juu ya Japan (JAXA).

Amesema hayo leo Oktoba 17, 2024 alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Kilele cha Kongamano la Nane la Mwaka la TEHAMA, lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Dar es Salaam.

“Katika eneo hili maandalizi ya utungwaji wa sera, sheria na uridhiwaji wa mikataba ya Kimataifa ya masuala ya anga za juu inaendelea.”Mheshimiwa Majaliwa ameitaka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari iwakusanye vijana wabunifu wenye uwezo wa kubuni teknolojia zenye manufaa kwa Taifa.

“Lakini simamieni hizi tafiti zenye kutoa matokeo na vijana hao waendelee kupewa fursa na kazi hizo ziingie kwa jamii na zianze kutumika.”

Pia Mheshimiwa Majaliwa ameiagiza Wizara ya Mawasiliano, Habari na Teknolojia ya Habari isimamie na kuhakikisha ujenzi wa Vituo vya Ubunifu (Innovation Hubs) katika mikoa iliyokubalika unafanyika kama ilivyopangwa.Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa mabadiliko ya kidijitali ni lazima na Safari hiyo haipaswi kumuacha mtu yeyote nyuma hususan kwenye mfumo wa kifedha jumuishi. “Kama mnakumbuka, Serikali katika mwaka 2020 ilizindua Mfumo wa N-Card ambao hadi kufikia sasa umefanikiwa kuwaunganisha wananchi wasiopungua milioni nne. Mfumo huo umesaidia sana kuokoa upotevu wa fedha katika vituo vya usafirishaji.”

Ameongeza kuwa mfumo huo umesaidia kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato. “Nitoe wito kwa Wizara kuhakikisha maeneo mengi ambayo Serikali imewekeza yanatumia mfumo wa N-card. Mfumo huo ni muhimu katika kuokoa upotevu wa fedha za Serikali na kuwasaidia wananchi kuacha kutembea na fedha taslimu na watumiefedha kwa njia ya kidijitali.”Katika hatua nyingine Mheshimiwa Majaliwa ameitaka Wizara ya Mawasiliano, Habari na Teknolojia ya Habari ihamasishe matumizi ya TEHAMA katika kutoa huduma, biashara na uzalishaji ili kuongeza uwazi, ufanisi na kuboresha maisha ya wananchi kiuchumi na kijamii;

Kwa Upande wake Waziri Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Jerry Silaa amesema kuwa Serikali imeendelea kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano ambapo kwa mwaka fedha 2023/24 jumla ya urefu wa kilomita 1,592 za mkongo wa taifa zimejengwa na kufika katika wilaya 83.

“Pia umoja wa watoa huduma za mawasiliano (consortium of telecom operators) wameweza kujenga jumla ya kilomita 2,595 ambazo zinafanya mkongo wa taifa kuwa na kilomita 13,820. Wizara imehamisha shughuli zote zinazohusiana na ujenzi wa mkongo wa taifa wa mawasiliano na kituo cha kuhifadhia data (NIDC) kwenda katika Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL).”
Naye, Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Afrika (AUDA-NEPAD) Bi. Nardos Bekele-Thomas amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada anazozifanya katika kuhakikisha Tanzania inatumia ukuaji wa sekta ya TEHAMA katika kuchagiza Maendeleo Endelevu nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news