DODOMA-Imeelezwa kwamba, Tanzania ipo mbioni kuanza uzalishaji wa madini ya Niobium ambayo ni moja ya madini adimu yanayotumika katika mitambo mbalimbali ikiwemo matumizi ya utengenezaji wa injini za Ndege na Roketi.
Hayo yamesemwa leo Bungeni na Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa wakati akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa jimbo la Mbeya Vijijini Mhe. Oran Njema kuwa ni lini uzalishaji wa madini ya Niobium na kiwanda cha uzalishaji wa Ferroniobium utaanza katika Halashauri ya Wilaya ya Mbeya.
Dkt. Kiruswa amesema kuwa, mradi wa uchimbaji wa madini ya Niobium katika eneo la Panda Hill unamilikiwa na kampuni ya Panda Hill Tanzania Limited (PHTL) kwa ajili ya uzalishaji wa mazao yanayotokana na madini hayo ikiwemo zao la madini ya ferroniobium linalotokana na uchakataji wa madini ya Niobium.
Aidha, Dkt.Kiruswa ameongeza kuwa, tayari Serikali imeanza majadiliano na kampuni ya Panda Hill kwa lengo la kusaini Mkataba wa Makubaliano utakaowezesha Serikali kupata umiliki wa hisa kwenye mradi huo ikiwa pamoja na manufaa mengine ya kiuchumi.

Dkt.Kiruswa amefafanua kuwa, utaratibu wa ulipaji wa fidia kwa waguswa wa mradi unaendelea vizuri pindi utakapokamilika taratibu za kuanza ujenzi wa kiwanda cha uchataji wa madini ya niobium utaanza rasmi.
Sambamba na matumizi katika nyanja ya sayansi ya teknolojia pia madini ya Niobium hutumika katika mitambo ya uchorongaji katika utafiti na uchakataji wa mafuta, gesi pamoja na utengenezaji wa magari.
Tags
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dr Steven Kiruswa
Habari
Niobium Minerals
Wizara ya Madini Tanzania