Tanzania na Iran zasaini Hati za Makubaliano kukuza diplomasia ya uchumi

DAR-Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Kiislam ya Iran zimesaini hati saba za makubaliano ili kukuza diplomasia ya uchumi baina ya mataifa hayo mawili.
Hafla ya kusaini hati hizo za makubaliano imefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam leo tarehe 19 Oktoba, 2024, katika mkutano wa tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano baina ya Tanzania na Iran.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo na Waziri wa Kilimo wa Jamhuri ya Kiislaam ya Iran, Mhe. Golamreza Nouri Ghezelcheh walishuhudia zoezi hilo la uwekaji saini hati hizo lililohusisha Wizara za Kisekta, baadhi ya Taasisi za Umma na Taasisi binafsi.

Akizungumza wakati akifungua mkutano huo uliohusisha Viongozi wa ngazi za juu za Serikali za nchi hizo, wakiwemo Mawaziri, Mhe. Balozi Kombo amemshukuru Mhe. Golamreza Nouri kwa jitihada zake za kuimarisha ushirikiano wa uwili na azma yake katika kuongeza maeneo ya ushirikiano yakiwemo biashara na uwekezaji, kilimo, nishati, ulinzi na usalama na elimu. Maeneo mengine ya ushirikiano baina ya Tanzania na Iran yatahusisha sekta ya afya, sayansi na teknolojia, na utamaduni.

Hati hizo za makubaliano zilihusisha hati ya makubaliano kati ya Wizara ya Kilimo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wizara ya Kilimo ya Jamhuri ya Kiislam ya Iran, kuhusu ushirikiano katika sekta ya Kilimo; Wizara ya Mifugo na Uvuvi ya Tanzania na Wizara ya Kilimo ya Iran kuhusu ushirikiano katika sekta ya afya ya wanyama; na hati ya makubaliano baina ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na Wizara ya Michezo na Vijana ya Iran.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news