Tanzania na Oman kushirikiana katika maeneo muhimu ya maendeleo

NA BENNY MWAIPAJA

TANZANIA na Oman zimekubaliana kuendeleza ushirikiano katika nyanja mbalimbali za maendeleo ikiwemo Sekta ya Nishati na Madini, kutengeneza mazingira bora ya uwekezaji, kubadilishana uzoefu na mafunzo katika masuala ya kodi pamoja na kuondoa utozaji kodi mara mbili kwa wawekezaji na wafanyabiashara watakaofanya shughuli zao kati ya nchi hizo mbili.
Hayo yamesemwa wakati wa kikao cha Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Oman nchini Tanzania, Mhe. Saud Al-Shidhani, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha jijini Dar es Salaam.
Mhe. Dkt. Nchemba, alisema kuwa ajenda kubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni kuhakikisha inawezesha sekta binafsi kuwa na nguvu, sambamba na uboreshaji wa mazingira ya biashara na uwekezaji, hivyo ushirikiano kati ya nchi hizo utaendelea kunufaisha sekta binafsi na wawekezaji kwa kiasi kikubwa.

“Serikali zetu mbili zimeanzisha Tume ya Kudumu ya Pamoja inayosimamia maeneo ya ushirikiano kati ya nchi zetu mbili, ikiwemo biashara na uwekezaji, hivyo natarajia kutakuwa na fursa ya kupanua zaidi ushirikiano wetu wa maendeleo kwa manufaa ya watu wetu,” alisema Dkt. Nchemba.Alikubali maombi ya Balozi wa Oman ambaye alisisitiza umuhimu wan chi yake kujifunza zaidi kuhusu mifumo ya kodi kutoka Tanzania kwa kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania ina uzoefu mkubwa katika aneo hilo na kwamba nchi yake imeanza kutoza kodi hivi karibuni.

“Tunatazamia Ushirikiano wa mafunzo hasa kwenye masuala ya kodi, na sehemu ambazo nchi zetu hizi mbili zina utaalamu mahsusi, lengo ni kujengeana uwezo pamoja ili tuweze kunufaika zaidi,” alisema Dkt. Nchemba.

Naye Balozi wa Oman nchini Tanzania, Mhe. Saud Al-Shidhani, ameipongeza Tanzania kwa kupiga hatua katika masuala ya kodi na ameona fursa ya kubadilishana uwezo katika masuala ya kodi ikiwa ni moja ya ajenda kubwa ya ushirikiano kati ya nchi hizo.Mhe. Balozi Al-Shidhani, alisema kuwa biashara kati ya nchi hizi mbili umeongezeka kwa kiasi kikubwa na kuna tija kubwa ya kuondoa utozaji kodi mara mbili kwa wawekezaji na wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao kati ya nchi hizo mbili.

“Tunapenda kusema kuwa Oman tunataka kujifunza namna ya kushughulikia masuala ya ukusanyaji wa mapato kwa Kuwa Tanzania tayari imepiga hatua katika masuala hayo na sisi tumeanza miaka ya karibuni, kwa hiyo tuna mengi ya kujifunza,” alisema balozi huyo.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Kamishna Msaidizi Idara ya Fedha za Nje Bw. Melckzedeck Mbise, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Sheria Wizara ya Fedha, Bi. Mwantumu Sultan na Maafisa wengine waandamizi wa Serikali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news