Tanzania tumepiga hatua kubwa masoko ya mitaji nchini-Waziri Dkt.Nchemba

NA GODFREY NNKO
Zanzibar

WAZIRI wa Fedha, Mheshimiwa Dkt.Mwigulu Nchemba amesema kuwa,juhudi zilizofanywa na Serikali kupitia Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) zimewezesha kufikiwa kwa maendeleo makubwa katika masoko ya mitaji nchini.
Ameyasema hayo leo Oktoba 1,2024 kupitia hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa 47 wa Mwaka wa Kamati ya Mamlaka za Usimamizi wa Bima,Masoko ya Mitaji na Huduma za Fedha zisizo za Kibenki (CISNA) jijini Zanzibar.

Hotuba ambayo imesomwa na Mheshimiwa Ali Suleiman Ameir, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu, Zanzibar.Wenyeji wa mkutano huo hapa nchini ni Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) wakishirikiana na Sekretarieti ya CISNA .

Amesema, juhudi hizo zimeiweka sekta ndogo ya masoko ya mitaji hapa nchini kuwa mojawapo ya vituo vikuu vya utoaji wa mitaji endelevu Afrika Kusini mwa Sahara.

"Soko hili limeongoza katika kutoa bidhaa za masoko ya mitaji zenye milengo mbalimbali zikiwemo hatifungani za kijinsia, hatifungani za kijani, hatifungani za uendelevu, na hatifungani za sukuk zinazokidhi sheria za Kiislamu.

Pia, Waziri Dkt.Nchemba amesema, baadhi ya mafanikio katika utoaji wa mitaji endelevu ni pamoja na hatifungani ya kwanza ya kijani iliyopewa jina la Kijani Bond ambayo ilikusanya shilingi bilioni 171.83 kufadhili miradi na biashara rafiki kwa mazingira, sawa na mafanikio ya asilimia 430.

"Vivyo hivyo, kutoa hatifungani ya kwanza ya Kijinsia iliyopewa jina Jasiri Bond iliyokusanya jumla ya shilingi bilioni 74.2 kufadhili biashara ndogo na za kati zinazomilikiwa na wanawake, pamoja na zile zinazomilikiwa na wanaume, lakini zenye matokeo chanya kwa wanawake."

Amesema,hatifungani hiyo ilipata mafanikio ya asilimia 297. "Aidha, soko la mitaji la Tanzania limewezesha utoaji wa hatifungani ya kijamii iliyotolewa kwa fedha mbalimbali iliyopewa jina la Jamii Bond ambayo ilikusanya shilingi bilioni 212.94 kufadhili miradi na biashara za uendelevu. Hatifungani hii ilipata kiwango cha mafanikio cha asilimia 284."
Vilevile, katika jitihada za kukuza upatikanaji wa fedha endelevu, Waziri Dkt.Nchemba amesema, masoko ya mitaji ya Tanzania pia yamewezesha utoaji wa hatifungani ya kijani ya kwanza iliyotolewa na mamlaka ya maji inayojulikana kama Hatifungani ya Maji Tanga.

"Hatifungani hii ilikusanya shilingi bilioni 54.72, sawa na mafanikio ya asilimia 103. Hatifungani ya Tanga ni bidhaa ya masoko ya mitaji yenye ubunifu, endelevu iliyotolewa na taasisi ya umma kwa ajili ya kugharamia miundombinu ya maji.

"Utoaji wa bidhaa za masoko ya mitaji endelevu hapa nchini unatoa msingi wa kubadilishana uzoefu miongoni mwa wanachama wa CISNA wakati wa mkutano huu."

Katika hatua nyingine, Waziri Dkt.Nchemba amesema kuwa, majanga yanayohusiana na hali ya hewa na mabadiliko ya tabianchi yanazidi kuwa ya mara kwa mara na makali kadri joto la dunia linavyoongezeka.

Amesema, hakuna bara au nchi iliyosalia bila kuguswa, huku mawimbi ya joto, ukame, vimbunga na tufani yakipelekea uharibifu mkubwa duniani kote.

"Mabadiliko ya tabianchi yanaweka changamoto nyingi katika jamii zetu, yakihusisha mifumo ya ikolojia, uchumi, jamii na ustawi wa binadamu.

"Kwa hiyo, udhibiti wa mabadiliko ya tabianchi na utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ni sehemu muhimu katika kukabiliana na changamoto za mazingira zinazoikabili dunia yetu leo.

"Kwa kuchukua hatua za makusudi za kuendeleza masoko ya fedha endelevu ili kugharamia mabadiliko ya tabianchi na kufanya kazi kuelekea kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu, nchi za SADC ziko katika nafasi nzuri ya kukuza ukuaji wa kiuchumi, ujumuishi wa kijamii na uendelevu wa mazingira kwa jumla."

Waziri Dkt.Nchemba amesema, katika kujibu changamoto hizo. "Sisi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tumetunga sera mbalimbali zikiwemo Mpango Kabambe wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (2022-2032) na Mpango Mkuu wa Maendeleo wa Sekta ya Fedha 2020/2021-2029/2030, unaoshirikisha sekta ya umma na binafsi."

Amesema,chini ya uongozi madhubuti wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar mambo makubwa yamefanyika.

"Tumepiga hatua kubwa katika maboresho ya kisera, kiudhibiti na kiutendaji kwa ajili ya ukuaji wa Sekta ya Fedha. Hatua hizi zimeleta chachu katika maendeleo ya Sekta ndogo za masoko ya mitaji, bima na huduma ndogo za fedha."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news