Tanzania yakoleza kasi mageuzi makubwa katika TEHAMA, kongamano la kihistoria kufanyika mwezi huu Dar

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Jerry William Silaa (Mb) amesema, Jamii Digital Innovation Hubs inalenga kuwawezesha vijana wenye bunifu, ujuzi katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kuweza kuyaendea malengo yao na kutimiza ndoto zao nchini.
Ameyasema hayo leo Oktoba 2,2024 jijini Dar es Salaam baada ya kukutana na uongozi wa Tume ya TEHAMA nchini (ICT Commission) chini ya Mkurugenzi Mkuu,Dkt. Nkundwe Mwasaga.

"Kwanza tumekutana na Tume ya TEHAMA (ICT Commission) ambayo imepewa mamlaka ya kisheria ya kusimamia sekta nzima ya ICT, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.

"Pamoja na kazi nyingi inazozifanya, ni kusimamia sekta nzima ya ICT na kuna mradi mkubwa unafanyika.
"Mradi wa Jamii Digital Innovation Hubs unafanyika kwenye mikoa nane, Dar es Salaam,Mwanza,Arusha, Mbeya, Dodoma, Tanga,Lindi na Zanzibar.

"Tunasema Jamii Digital Innovation Hubs ni maeneo ambayo kwa sababu katika kazi wanazofanya vile vile Tume ya TEHAMA ni kuchochea Start-ups.

"Kampuni za wabunifu, wako vijana wengi wanaosomea masuala ya IT, wengine wana-graduates,wengine ni wabunifu tu ambao wanataaluma mbalimbali, lakini sasa anafanyaje kazi.

"Ubunifu wake anaufikishaje kwenye biashara,kwa hiyo Serikali ya Dkt.Samia Suluhu Hassan kupitia Mradi wa Digital Tanzania inafadhili Mradi wa Jamii Digital Innovation Hubs kwenye hayo maeneo nane niliyoyataja.
"Ili vijana wenye ubunifu, vijana wenye ujuzi, vijana wenye wazo wapate sehemu ya kuwa na kaofisi, kupata zile huduma za kufungua kampuni, na kuanzisha biashara, kukaa pale kwa angalau miezi nane.

"Maana leo akisema atoke na wazo lake,intaneti atapata wapi,ofisi ya kupangisha, hizo pesa anatoa wapi.

"Serikali ya Dkt.Samia Suluhu Hassan imeanzisha Hubs hizi ili ziweze kumsaidia huyo kijana akiwa na wazo lake, akiwa na ubunifu wake apate kasehemu kwa kwenda kukaa, kupata huduma za kisheria.

"Kufungua kampuni na vitu vingine na kulichakata lile jambo lake kupata wadau ambao wanaweza waka-test zile huduma zake za ICT kwenye mifumo yao ikiwezekana ziweze kuzalisha fedha na ziweze kumpatia ajira na yeye aweze kuajiri wenzake.

"Ninyi nyote mtafahamu kwamba ICT Commission kwa kushirikiana na wadau mbalimbali hata maeneo wanakokwenda kufanya hizi Innovation Hubs wanafanya ushirikiano na SIDO.

"SIDO ni taasisi yetu, mnafahamu inafanya kazi kubwa sana katika kuchochea ujuzi, kuchochea ujasiriamali na ICT ambayo inafanyika.

"Jambo lingine, ICT Commission inafanya makongamano mbalimbali kila mwaka na wiki mbili zijazo unafanyika mkutano mkubwa wa ICTP.
"Mkutano huu unaleta wadau wote wa Sekta ya ICT, kukutana pamoja na kujadiliana uzoefu, kuweza kuzungumza mambo mbalimbali yanayotokea kwenye upande wa TEHAMA,

"Lakini vilevile kuendelea kuhabarisha umma innovation mbalimbali na maendeleo mbalimbali katika sekta ya TEHAMA.

"Nyote mnafahamu sasa hivi,Dunia nzima inazungumzia masuala ya Artificial Intelligence (Akili Mnemba).

"Artificial Intelligence ni teknolojia ambayo inafanya kazi kubwa sana ya kompyuta kufikiri kama anavyofikiri binadamu.

"Na imeanza kutumika nchini, ni kitu kigeni na ni kitu ambacho kimeshika kasi na yenyewe ilikuwa ni kati ya maeneo ambayo ICT Commission inasimamia.

"Na itaandaa mkutano maalum kwa ajili ya kubadilishana uzoefu wa wataalamu mbalimbali wa sekta ya ICT kwenye eneo la Artificial Intelligence.

"Kwa hiyo kazi wanayofanya ni kubwa na sisi kama wizara wakati wote tutaendelea kuwaunga mkono na kushirikiana nao katika kuwawezesha, kuwasaidia kuwasemea ili malengo yaliyolengwa wakati tume hii inaanzishwa yaweze kufikiwa."

Waziri Silaa ameeleza kuwa, Innovation Hubs imelenga kuwanufaisha vijana wengi zaidi nchini.

Amesema, kupitia kongamano hilo anatarajia vijana na washiriki wengine kupata uelewa wa kutosha kuhusu teknolojia.

"Kwa sababu teknolojia inakuwa kwa kasi,kwa hiyo ni jambo jema la watu kukutana, kuona tulikotoka, tuliko na tunakokwenda,"amesisitiza Waziri Silaa.

ICT Commission

Dkt. Nkundwe Mwasaga ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA nchini amesema kuwa, kongamano la nane ambalo Tanzania imepata bahati ya kuliandaa lina umuhimu mkubwa.

"Cha kwanza kuna kongamano lenyewe la TEHAMA la nchi, lakini kwa mara ya kwanza kwa Afrika kuna mashindano ya Akili Mnemba na Roboti ya Vijana ukanda wa Afrika. Kwa mara ya kwanza yanazinduliwa Tanzania.

"Sasa, hili kongamano na hayo mashindano yanafanyika Dar es Salaam katika Ukumbi maarufu wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere na kongamano hilo litaanza tarehe 13 hadi 17 Oktoba,2024.
"Kongamano hili lina mambo mengi, kwanza lina mada nyingi ambazo wataalamu mbalimbali watakuwa wanajadiliana pamoja na wataalamu wetu wa Kitanzania.

"Pia, kuna mambo ya maonesho, katika mambo ya maonesho tuna maonesho ya kampuni ndogo ndogo yaani hizi start-ups za vijana wa Kitanzania na watu wa nje ambao wataonesha teknolojia mbalimbali.Lakini,pia ni fursa."

Dkt.Mwasaga akizungumzia kuhusu idadi ya nchi anbazo zimethibitisha kushiriki kwenye kongamano hilo ni pamoja na mataifa yote ya Umoja wa Ulaya.

Pia, kuna nchi mbalimbali za Afrika kwa maana ya Umoja wa Afrika,Marekani, China,nchi za Mashariki ya Kati ikiwemo Japan.

"Kwa hiyo hili kongamano ni kongamano lenye sifa za sura ya Kimataifa.

"Na sisi, tunajivunia sana kwa wizara yetu kuweza kufanya kazi bega kwa bega na Tume ya TEHAMA kuhakikisha kwamba hili jambo linakuwa kubwa.

"Kwa sababu hili si jambo si mkutano wa kawaida, huu mkutano unahusisha uhusiano wa Kimataifa, hivyo tunatakiwa tuihusishe wizara ili kuleta mialiko mbalimbali na ili tuweze kufanikisha vizuri.

"Sisi, tuko tayari katika kuhakikisha hili jambo linafanikiwa na kuifanya Tanzania kuwepo kwenye ramani ya Dunia.

"Katika kutambua kuhusu kuwepo kwa changamoto hasa vijana ambao wananaliza katika vyuo au vyuo vya VETA au hata wanaomaliza shule.

"Wengi wanakuwa wana bunifu zao, wanazo nyingine wanazifanya kama project ya mwaka wa mwisho wa masomo yao au wengine ni wabunifu tu wanatengeneza bidhaa zao.

"Sasa tuliangalia changamoto gani wanakutana nazo, kuna changamoto nyingi moja wapo, moja wapo ni changamoto ya kuwa na ofisi na kuweza kuilipia.
"Kwa hiyo, kwa kuliona hivyo,Serikali ya Dkt.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikaona kwamba ni vizuri itengeneze project.

"Project ambayo itatengeneza vituo kila mikoa kwa kuanza na vituo vinane vya mikoa nane, lakini ndani yake kuna vituo 10."

Amesema, hivyo vituo vitakuwa vinatoa nafasi kwa wale ambao wanafika na bunifu zao kukaa kwa miezi nane.

"Katika hiyo miezi nane,anajengewa uwezo wa mambo mbalimbali wa kibenki, wa kisheria, wa kupata haki ya hizo vumbuzi zao."

Pia, amesema atapata nafasi ya kutumia bodi room kama ya kwake ikiwemo kutumia vifaa vyote.

"Ili hizo bunifu zao kuweza kuzijenga sasa kuwa kampuni. Akikaa miezi nane, yeye atatoka halafu atatengeneza nafasi kwa watu wengine waweze kuingia wapate hizo nafasi.

"Lakini, sasa tumeangalia tukaona kuwa si tu wabunifu wanatengeneza software.

"Katika hivyo vituo 10, vituo viwili ni vya kutengeneza au kuunda vifaa vya TEHAMA.Kwa hiyo, kimoja kitakuwa Dar es Salaam na kingine kitakuwa Arusha ambapo kazi yake yenyewe ni kutengeneza.
"Kwa hiyo, wale ambao wamejiajiri mfano ku-repair vifaa vya TEHAMA watapata nafasi ya kuweza kupata vifaa ambavyo saa nyingine ni ngumu kwa yeye mwenyewe kuweza kununua au kupata components ambazo zitawasaidia kufanya kazi zao.

"Kwa hiyo, sisi wote tumeangalia haya kukuza au kutengeneza chachu ya masuala ya ubunifu kwenye TEHAMA.

"Na tumeangalia kwamba, kwa hali ya sasa hivi ilivyo, Dar es Salaam ndiyo sehemu pekee ambayo tunaona kuna watu wengi wamefanikiwa sana kwenye TEHAMA.

"Kwa hiyo, tumeamua kufanya hivyo Lindi na mikoa ambayo inazunguka Lindi. Mbeya, Mwanza, Arusha, Tanga,Dodoma, Dar es Salaam na Zanzibar kwa kuanzia.

"Lakini, pia tuna mradi mwingine ambao unatengeneza vituo si vikubwa sana kama hivyo, lakini vya size fulani katika kila wila

"Kwa hiyo tumeanza na tunategemea kwamba muda unavyojwenda tutafika huko.

"Na pia, tumetengeneza tena mradi mwingine kwa kutengeneza maabara za kompyuta kwenye shule za kata kwa kutumia wanafunzi ambao walipita katika shule hizo.

"Au wanaotoka katika maeneo hayo ambao wanafahamika kama Alumin, tunawatumia Alumin kutengeneza maabara za bei nafuu sana."

Amesema, katika kongamano hilo wametengeneza wasilisho ambalo wataonesha jinsi maabara hizo zitakavyokuwa na namna watakavyotumia watu wa eneo fulani au waliosoma shule fulani kuweza kutengeneza hizo maabara ili kusaidia wanafunzi.

"Kwa hiyo,tuna plan kubwa za kutengeneza ujuzi Watanzania wote na vile vile kufikisha mambo ya ubunifu kwa njia hizo tatu.

"Kufika katika ngazi ya wilaya, kufika katika shule za kata ili kutengeneza vituo vikubwa zaidi ambavyi vyenyewe vimechagiza masuala ya Start-up kuweza kuifanya Tanzania kuwa shindani kwenye uchumi wa digitali."

Pia,amesema miongoni mwa sababu zilizoifanya Tanzania kupewa nafasi kuandaa kongamano hilo pamoja na uimara katika usalama wa mitandao.
"Kuna vitu fulani ambavyo vimeonesha kabisa Tanzania tupo tayari, kwa mfano tukiangalia jinsi tunavyopimwa duniani.

"Kuna Tathimini ambayo imetoka mwezi uliopita (Septemba) imetupima katika mambo ya usalama mtandao duniani katika kuwa nafasi ya kwanza.

"Na katika watu ambao waneongoza nafasi ya kwanza wanaita T1 ziko nchi 46 tu na ndani ya hizo nchi.Sisi Tanzania tuliweza kupata alama 99.27, kw hiyo katika eneo hilo tunafanya vizuri.

"Katika masuala ya kutoa huduma za kidigitali tupo katika nchi bora 25 na na hiyo tumetathiminiwa na watu wengine na ukiangalia mambo ya Start-up yanakuwavizuri.
"Kwa hiyo,Tanzania imeonesha mwelekeo mkubwa duniani kwamba tunauwezo wa mambo mengi.

"Ndiyo maana kwa kuangalia na mambo mengine yanayosaidia kwa maana ya usalama na amani ya nchi yetu waneona kwamba ni sehemu nzuri ya kufanyia hayo mashindano hapa.

"Na sisi tumefurahi sana. Kwa sababu tumeweka historia kwa Afrika kwa sasa tunaanza kutambulika kuwa ni nchi ambayo inatumika katika teknolojia na inawagusa vijana wa Afrika."

Akizungumzia kuhusu masuala ya Akili Mnemba, Dkt.Mwasaga ameeleza kuwa, "Kwenye masuala ya Akili Mnemba, Tanzania tena katika tathmini ya Dunia, inafanya vizuri.

"Sasa, Akili Mnemba matumizi yake yako ya aina mbili, kuna yale matumizi ya kawaida ambayo mtu yeyote mwenye simu janja kwenye hiyo simu tayari Akili Mnemba ipo na kwenye matumizi karibia wote tunatumia.

"Lakini, katika matumizi makubwa ya kiserikali kwa Afrika, Mahakama ya Tanzania ndiyo imekuwa katika mahakama za mwanzo ambazo zinatumia Akili Mnemba katika shughuli zao za kawaida. Hilo jambo limewashangaza watu wengi.
"Lakini, huo ndiyo ukweli Mahakama ya Tanzania inatumia hiyo, kuna viwanda viko Tanzania kwa sasa hivi vinatumia sana Roboti na Akili Mnemba kwenye kufanya mambo ya utengenezaji.

"Kwa hiyo ukiangalia kwa ujumla wake hata vyuo vyetu vinatoa machapisho mengi sana ya Akili Mnemba.

"Kwa hiyo hayo yote yanaonesha wazi kwamba tuko tayari na sisi tuko mbioni kutengeneza Kituo cha Afrika cha Mambo ya Akili Mnemba na Roboti ambacho kitasaidia nchi nyingine mbalimbali za Afrika kuweza kufikia katika ndoto yetu kama nchi,"amesema Dkt. Nkundwe Mwasaga.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news