Tanzania yazidi kuziacha nchi nyingi Afrika kidijitali

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Jerry Silaa amefungua kikao kazi cha siku tatu ambacho kimejikita kufanya mapitio katika maeneo 11 ambayo nchi za Afrika zilijiwekea awali katika Mkutano wa Dunia wa Jumuiya ya Habari (WSIS).
Mheshimiwa Waziri Silaa amefungua kikao kazi hicho leo Oktoba 9,2024 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam

Kikao kazi hicho ambacho kinatarajiwa kufikia tamati Oktoba 11,2024 kimeandaliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Kamisheni ya Umoja wa Mataifa (UN) kuhusu Uchumi wa Afrika (ECA).

Aidha, kupitia kikao kazi hicho ambacho kimewaleta pamoja watunga sera, wataalamu, na wadau kutoka Afrika na nje ya Afrika kinafanya tathmini ya mafanikio na mapungufu katika utekelezaji wa mikakati waliyojiwekea katika miongo miwili iliyopita na kuimarisha ushirikiano wa kujenga jamii ya kidijitali shirikishi na endelevu.
"UNECA ambayo inashughulika na masuala ya ICT, miaka 20 iliyopita mwaka 2003 Geneva na mwaka 2005 Tunis kulifanyika mkutano unaoitwa WSIS ambapo mwakani itakuwa ni WSIS +20 ambayo ni miaka 20 baada ya mkutano huo.

"Mkutano huo uliweka actions 11 kwa ajili ya kuwezesha ama nchi za Afrika ziweze kujipanga kwenye masuala ya kidijitali.

"Kikao kazi hiki kimekuja kufanya mapitio ya kuona yale maeneo 11 ambayo nchi za Afrika zilijiwekea wamefikia wapi, wana changamoto gani,kuna yapi ya kujifunza kwa ajili ya kuelekea mkutano wa mwakani."

Kwa mujibu wa Waziri Silaa, miongoni mwa maeneo hayo ni upatikanaji wa taarifa na maarifa kwa wote kuanzia ngazi ya Taifa hadi Kimataifa.

Pia, eneo lingine likiwa ni kuhimiza na kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na jamii ili kufikia mawasiliano jumuishi na endelevu.

Vilevile, katika mkutano huo walikubaliana kuhusu kuendeleza miundombinu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuhakikisha hakuna kundi ambalo linaachwa nyuma.
Jambo lingine ni kuhusu umuhimu wa kujenga ujuzi na uwezo wa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Suala lingine amesema ni kuhusu kuimarisha usalama wa mtandao na ulinzi wa taarifa binafsi, ambapo amesema upande huu Tanzania imepiga hatua kubwa zaidi.

Mbali na hayo, pia walikubaliana kuendeleza ushirikiano wa kimataifa na wa kikanda ili kuifanya jamii ya habari kuwa yenye manufaa na endelevu.

Eneo lingine linasisitiza mifumo imara ya kisheria na kanuni zinazosaidia matumizi ya TEHAMA.

Aidha, kuifanya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kuwa msingi imara katika kuwezesha sekta zingine ikiwemo Serikali Mtandao (e-Government),elimu, afya na nyinginezo.

Mambo mengine ni kuhusu masuala ya kitamaduni katika zama za kidijitali,jukumu la vyombo vya habari katika jamii ya habari na umuhimu wa uhuru wa kuzungumza ikiwemo athari za kimaadili kwa jamii kupitia TEHAMA.
"Lakini, workshop hii inafanyika wakati tayari Tanzania, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ameshazindua Tanzania Digital Economy Framework (Mkakati wa Tanzania ya Kidigitali wa Miaka 10) kuanzia 2024 hadi 2034."

Waziri Silaa amesema, pamoja na mambo mengine mkakati huo unaonesha jinsi gani nchi yetu itajumuisha masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwenye uchumi na masuala ya kijamii.

"Lakini, yapo mengi Serikali imefanya, uwekezaji mkubwa kwenye miundombinu ya TEHAMA, tunao Mkongo wa Taifa.

"Uwekezaji mkubwa kwenye minara ya mawasiliano,sheria mbalimbali, sera mbalimbali kwa ajili ya kuhakikisha Tanzania inaendelea kushiriki na nchi nyingine katika uchumi digitali.

"Lakini, kwenye jarida la Muungano wa TEHAMA Duniani lililotoka mwezi Septemba, Tanzania imetajwa kama moja ya nchi 49 vinara kwenye masuala ya Usalama Mtandao.

"Na katika nchi hizi za Kiafrika, Tanzania imeibuka namba moja kwa hiyo si tu kwenye masuala ya uwekezaji wa Tume ya TEHAMA na miundombinu kwa maana ya connectivity na covereges. Lakini, vile vile hata kiutendaji tuko vizuri."

Pia, amesema kikao kazi hicho kimekuja ikiwa wiki ijayo Kongamano la Kihistoria la TEHAMA linatarajiwa kufanyika hapa nchini.

"Mkutano huu umefanyika Tanzania kati ya nchi nyingi za Afrika, lakini vile vile umefanyika kwenye nchi ambayo na yenyewe kwa maelezo ya Mheshimiwa Rais na kwa kazi nzuri ambayo anaifanya tupo vizuri katika TEHAMA,"amefafanua Waziri Silaa.
Mkuu wa Idara ya Ubunifu na Teknolojia wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa (UN) kuhusu Uchumi wa Afrika (ECA), Dkt.Mactar Seck amesema, maeneo hayo 11 watayafanyia mapitio ya kina ili kuja na yatokanayo ambayo ni muhimu kwa mkutano ujao wa WSIS+20.

Amesema,matokeo ya kikao kazi hiki cha siku tatu yataandaliwa ripoti ya kina ya mapitio itakayotoa mapendekezo ya sera kwa ajili ya kuongeza utekelezaji wa WSIS barani Afrika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news