TEF yatoa tamko TCRA kuifungia mitandao ya kijamii Mwananchi Communications Limited

DAR-Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limeeleza kushtushwa na taarifa za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kusitisha kwa siku 30 leseni za huduma za maudhui mtandaoni za Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (The Citizen, Mwananchi Digital, Mwananchi na MwanaSpoti).
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Oktoba 3,2024 na Deodatus Balile ambaye ni Mwenyekiti wa TEF.

Balile amesema, sheria iliyotumika kufungia huduma ya maudhui mtandaoni ya The Citizen, Mwananchi Digital, Mwananchi na MwanaSpoti yanayomilikiwa na MCL, ni ile ile inayolalamikiwa kwa muda mrefu.

Taarifa ya kufungiwa kwa maudhui hayo ilitolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dkt. Jabiri Bakari tarehe 2 Oktoba,2024.

"Taarifa hiyo inasema, kampuni hiyo ilichapisha maudhui yaliyokiuka kanuni ambayo yameleta tafsiri hasi kwa taifa, jambo ambalo linaathiri na kuharibu umoja, amani na mshikamano wa kitaifa,” imeeleza taarifa ya TEF.

Akifafanua kadhia hiyo katika taarifa hyo, Balile ameeleza kwamba, kwa muda mrefu TEF imekuwa ikilalamikia mamlaka makubwa yanayotolewa kisheria kwenye taasisi au wakuu wa taasisi ya kuwa walalamikaji, waendesha mashitaka na watoa hukumu bila upande wa pili unaotuhumiwa kupewa fursa ya kusikilizwawazi hadharani.

“Tutaendelea kudai haki hii ya asili (natural justice) ya chombo cha habari kinachotuhumiwa kupewa hati ya mashitaka, kikajitetea mbele ya taasisi huru au Mahakama, kisha uamuzi ufanyike ambao ndiyo utawala wa sheria badala ya sasa ambapo, sheria inatoa mamlakakwa mtu mmoja kufanya uamuzi mzito kama huu.

“Mwananchi walipaswa kufunguliwa mashataka katika chombo huru na wao kujitetea, kisha chombo hicho kutoa hukumu kulingana na mashtaka yaliyowasilishwa mbele yake,” imeeleza taarifa hiyo.

Hata hivyo, Balile amewasihi wahariri na watendaji wa vyombo vya habari kufahamu kuwa, sheria mbaya inaendelea kuwa sheria hadi itakapobadilishwa.

“Tunawasihi wahariri na waandishi nchini kufahamu ukweli kuwa utamaduni unatofautiana nchi hadi nchi, na zipo njia za kufikisha ujumbe kwa njia sahihi badala ya kujiingiza katika mazingira yanayoweza kutafsiriwa kama kejeli,” imeeleza taarifa hiyo.

Amesema, kwa vyovyote vile, tayari tatizo limetokea na kinachotakiwa sasa tunashauri pande zote mbili; Serikali na Mwananchi Communications, wakutane na kujadili suala hili na kulimaliza kwa masilahi mapana ya taifa na uhuru wa vyombo vya habari ndani ya muda mfupi kadri inavyowezekana.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news