DAR-Wazalishaji wa mbolea nchini wametakiwa kutumia malighafi za kutengeneza mbolea zinazopatikana ndani ya nchi ili kupunguza gharama za uzalishaji kwa kuagiza malighafi hizo kutoka nje ya nchi.
Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Joel Laurent (kulia) akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni la mbolea Yara Tanzania Limited, Winstone Odhiambo wakiangalia aina za mbolea zinazozalishwa na kampuni hiyo wakati wa ziara kwenye kiwanda hicho kilichopo Kurasini Jijini Dar Es Salaam leo Oktoba 3, 2024.
Wito huo umetolewa leo Oktoba 3, 2024 na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Joel Laurent alipofanya ziara kwenye kiwanda cha kuchanganya mbolea cha kampuni ya mbolea ya Yara Tanzania kilichopo Kurasini jijini Dar es Salaam.
Akieleza lengo la ziara hiyo, Mkurugenzi Laurent amesema, ni moja ya majukumu ya mamlaka kutembelea wadau wake ili kujiridhisha na uwezo wa uzalishaji wa viwanda vilivyopo nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni la mbolea Yara Tanzania Limited, Winstone Odhiambo akifafanua jambo kwaMkurugenzi Mtendaji wa TFRA na Viongozi na watendaji alioambatana nao kwenye ziara ya kikazi kiwandani hapo leo Oktoba 3, 2024.
Laurent amewataka waingizaji wa mbolea nchini kuwekeza katika viwanda vya kuchanganya mbolea ili kuwawezesha wakulima kupata mbolea inayoendana na mahitaji ya zao pamoja na aina ya udongo unaolimwa na si kutumia mbolea kimazoea.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mbolea ya Yara Tanzania Limited, Winstone Odhiambo amesema, kampuni yake inajikita katika kuzalisha mbolea kulingana na mahitaji ya wakulima ili kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo hiyo kwa wakati na ubora unaokubalika kimataifa.
Amesema, mpaka sasa wamewekeza kwenye mitambo miwili ya kuchanganya mbolea yenye uwezo wa kuzalisha tani 120 kwa saa na hivyo kuwahakikishia uwezo wa kuzalisha tani 720,000 kwa mwaka.
Kwa upande wake Meneja wa kiwanda, Santus Chonya amesema, wanazalisha aina mbalimbali za mbolea kulingana na mahitaji ya wakulima wanayoyabaini baada ya kupima udongo na kujua mahitaji ya virutubisho yanayolingana na aina ya zao linalolimwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Joel Laurent (katikati) akiwa katika picha na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mbolea ya Yara Tanzania Ltd kulia kwake na wataalam wa pande zote mbili ikiwa ni ziara ya kawaida yenye lengo la kujua hali ya uzalishaji na upatikanaji wa mbolea ilivyo nchini leo Oktoba 3, 2024.
Amezitaja mbolea hizo kuwa ni micro planting (mbolea ya kupandia), micro mbogamboga,micro top (mbolea ya kukuzia) na micro tobacco zinazofanya kazi vizuri kwenye mazao yaliyokusudiwa.
Naye Mkurugenzi wa Uzalishaji wa Ndani na Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja wa TFRA, Louis Kasera ameeleza kuwa, ziara hiyo inaipa picha halisi mamlaka ya kutambua uwezo wa nchi katika kuhudumia wananchi wake kwa kuwafikishia pembejeo hiyo kwa wakati.
Amewatoa hofu wananchi wanaoamini kuwa mbolea inaharibu udongo na kueleza mbolea ni chakula cha mmea kinachopaswa kutumika kwa usahihi ili kuwapa tija wanayoitarajia.
Ziara hiyo ni mwendelezo wa maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Mbolea Duniani yanayotarajiwa kufanyika kuanzia Oktoba 10 hadi 13, 2024 katika mikoa ya Manyara na Dodoma.